Bodi ya Mkonge Tanzania (TSB), imetoa ufafanuzi kuhusu usambazaji na upatikanaji wa mbegu za mkonge ambapo imezitaka Amcos kutochangisha wakulima fedha kwa ajili ya usambazaji wa mbegu hizo.
Aidha, imesema mbegu zitamfikia mkulima hadi alipo bila gharama yoyote.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Mkonge, Saddy Kambona ametoa kauli hiyo jana baada ya kikao na ukaguzi wa Shamba la Kibaranga (Kibaranga Sisal Estate) lililopo wilayani Muheza mkoani Tanga.
Kambona amesema serikali imeipatia Bodi ya Mkonge fedha kwa ajili ya mbegu na zitasambazwa kwa wakazi wote wa Kibaranga na kwa maelekezo ya serikali mbegu zitamfikia mwananchi kwenye kijiji chake bila kuchangia gharama yoyote.
“Kwa hiyo kama mlikuwa mna makubaliano kwamba mbegu zifike hapa Kibaranga Makao Makuu lakini ikatokea uhitaji Kijiji cha Darajani mkafanya utaratibu wa wananchi kuchangia ili mbegu zipelekwe kule na nadhani hatua muhimu ni mpate mawasiliano na Mkurugenzi Bodi ya Mkonge kwani Ofisi ya Mkurugenzi inao wajibu wa kuhakikisha kwamba mbegu zinazokusanywa katika awamu inayofuata zinafikishwa Darajani.
“Asichangishwe fedha mwananchi yeyote wa Darajani ili kupata mbegu labda kama mnafanya masuala mengine ya ulinzi wa mbegu na vitu kama hivyo, lakini si gharama za kufikishiwa mbegu Kijiji cha Darajani au kijiji chochote kingine.
“Bodi ya Mkonge itafikisha hizo mbegu huko ili wananchi waweze kulima mkonge, kule ambako mbegu zinatakiwa zifike zitafika asichangishwe mtu fedha,” alisema Kambona.
Awali mwenyeki wa Kijiji cha Darajani, Makende Maziku alisema wakulima wa mkonge katika kijiji hicho wamepokea ofa ya mbegu za mkonge vizuri na kusisitiza kasi zaidi ya upatikanaji wa mbegu hizo.
“Ofa ya mbegu tumeipokea vizuri lakini kuwe na kasi ya sasa ni ndogo mno kwani kila siku mahitaji ya mbegu yanaongezeka wengine tunashindwa kuchukua kwa sababu hawa tulio nao sasa hivi hawajapata waliopata ni wachache,” alisema.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Amcos ya Kibaranga, Paulo Haule alisema utaratibu uliokuwapo ni kuwa mbegu zinaishia Makao Makuu ya Amcos.
“Maelekezo tuliyo nayo ni kuwa mbegu ziishie makao makuu lakini Mwenyekiti wa Kijiji cha Darajani alikubaliana na watu wake ikifika zamu yao kusambaziwa mbegu hizo wachangie mafuta kama gharama ya usafiri na mlinzi wa eneo hilo wanamlipa kiasi kidogo basi wanafikishiwa mbegu,” alisema.






0 Comments