Na Amon Mtega, MatukioDaimaAPP
Songea
MWENYEKITI wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Tanzania Hamis Livembe ameiomba Serikali kuona namna ya kuondoa mlundikano wa kodi mbalimbali kwenye biashara na kuziweka kwenye kapu moja.
Ombi hilo amelitoa kwenye mkutano wa wafanyabiashara wa Mkoa wa Ruvuma ambao mgeni rasmi alikuwa Naibu katibu mkuu wa Wizara ya Uwekezaji,Viwanda na Biashara Dkt,Hashil Twalib Abdallah .
Akizungumza kwenye mkutano huo mwenyekiti Livembe amesema kuwa licha ya Serikali ya awamu ya sita kuweka mfumo wa ulipaji kodi kwa hiyali bila kusulutishwa ila kumekuwepo na changamoto ya mrundikano wa kodi kutoka kwenye baadhi ya taasisi na kupatiwa mamlaka za kukamata na kuhukumu.
Livembe amesema kuwa kama mrundikano wa kodi hizo zikiwekwa kwenye kapu moja badala ya kila mamlaka kupita kujikusanyia basi itawasaidia wafanyabiashara kuwaondolea mzunguko wa ulipaji kodi ambazo mara zote wamekuwa wakizilalamikia.
Amesema kuwa kuna baadhi ya mamlaka zimekuwa zikiwahukumu Wafanyabiashara bila hata kuwapeleka kwenye vyombo vya sheria jambo ambalo limekuwa likiwanyanyasa wafanyabiashara hao.
Kwa upande wake mjumbe wa bodi ya Wafanyabiashara taifa Safieli Msigira wakati akitoa neno la shukurani kwa Naibu katibu mkuu wa Wizara ya Uwekezaji Viwanda na Biashara Dkt,Hashil Twalib Abdallah amesema kuwa inashangaza kuona baadhi ya wafanyakazi wa mamlaka ya mapato kuwapigia simu kwa baadhi ya Wafanyabiashara kuwadai walipe kodi za nyuma wakati Rais Samia Suluhu Hassan alishatoa maelekezo kuwa kodi za nyuma waziache waanze ukurasa mpya wa ukusanyaji wa kodi.
Nanye mwenyekiti wa wafanyabiashara Mkoa wa Ruvuma Tito Mbilinyi wakati akifungua mkutano huo amesema kuwa Serikali ya awamu ya sita inaonyesha mwanga wa namna ya kuwajali Wafanyabiashara jambo ambalo litasaidia kulipa kodi kwa hiyari na kuwafanya Wafanyabiashara wadogo nao kukua kibiashara.
Aidha Naibu katibu mkuu wa Wizara ya Uwekezaji Viwanda na Biashara Dkt,Hashil Twalib Abdallah amewapongeza Wafanyabiashara hao kwa kutambua mchango unaofanywa na Serikali juu ya kuwajali Wafanyabiashara hao .
Hata hivyo Naibu katibu mkuu huyo amewataka Wafanyabiashara wa Mkoa wa Ruvuma kutumia fursa zilizopo kwa kuanzisha Viwanda vidogo vidogo pamoja na Viwanda vikubwa kutokana na Mkoa huo kuwa na eneo kubwa la Uwekezaji.
Mwisho.









0 Comments