Na Gift Mongi,Matukio DaimaAPP
,Moshi
Katika kuunga mkono jitihada za kutangaza utalii wa ndani kama ulivyoasisiwa rais Samia Suluhu Hassan kupitia filamu ya The Royal Tour balozi wa utalii Lyidia Lukuba, ameandaa matembezi katika vivutio vya asili vya utalii vilivyopo katika hifadhi ya mlima Kilimanjaro.
Balozi huyo anaandaa matembezi hayo lengo likiwa ni kuhamasisha utalii wa ndani lakini pia kutambulisha aina mpya ya vivutio ambavyo kwa namna moja ama nyingine vinaonekana kusahaulika ambavyo vipo ndani ya hifadhi hiyo.
Akizungumza mjini hapa na waandishi wa habari Balozi Lyidia alisema matembezi hayo pia ndani yake yatahusisha mbio za baiskeli ambapo pia ni kivutio kingine katika kuhamasisha utalii.
"Utalii hufanywa kwa njia mbali mbali lakini naomba kuwajulisha katika matembezi haya yatahusisha pia mbio za baiskeli kilomita 40 na zitaenda kuanza katika geti la Marangu hadi kituo cha Mandara ndani ya hifadhi ya mlima Kilimanjaro"alisema balozi huyo
Kwa mujibu wa balozi huyo matembezi hayo yenye jina la Marangu Nature walk, yatahusisha vivutio vya kitalii vilivyopo kijiji cha Marangu sanjari na uwepo wa vyakula vya asili na vinywaji vya asili ya kabila la wachagga
Aliongeza kuwa matembezi ya kilomita 5 yatafanyika katika kivutio cha utalii cha Ndoro Walter falls na kumalizikia kwa kwa Hosea wakati yale ya kilomita 10 ya tamalizikia Kinukamori na kuwa matembezi haya yanatarajiwa kufanyika julai 10 mwaka huu ambapo mgeni rasmi atakuwa naibu waziri wa maliasaili na utalii Marry Masanja.
"Mwakani pia matembezi haya yatafanyika japo inaweza zisiwe tarehe kama hizi lakini kila tunapofanya watu wanazidi kuhamasika na haya ni mafanikio makubwa katika utalii"alisema
Kwa upande wake Victus Mganza ambaye ni afisa uhifadhi katika hifadhi ya taifa Kilimanjaro alisema balozi huyo amehamasisha utalii wa ndani na hivyo ni jambo la kuigwa kwa kuungwa mkono na watu mbalimbali.
"Tumeshuhudia uhamasishaji utalii unavyofanywa na balozi huyu hivyo naona ni jambo ambalo ni nzuri na linalofaa kuungwa mkono kwa mafanikio kwenye sekta yetu hii"alisema
Mwisho.
0 Comments