Na John Gagarini Kibaha
MKOA wa Pwani umewataka watafiti wa Kilimo nchini kuwapatia wakulima matokeo ya tafiti wanazofanya ziweze kuleta mabadiliko kwa wakulima ili waende kwenye kilimo biashara na siyo cha kujikimu.
Hayo yalisemwa na mkuu wa Wilaya ya Kibaha Sara Msafiri ambaye alimwakilisha mkuu wa mkoa wa Pwani wakati wa maadhimisho ya siku ya Mkulima yaliyoandaliwa na Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) Kibaha.
Msafiri kuwa watafiti hao wanapaswa kutumia tafiti hizo kwa vitendo kwa wakulima ambapo serikali imetenga bajeti kubwa ambayo haijawahi kutokea na imeonyesha jinsi gani serikali ilivyotoa kipaumbele kwenye sekta ya Kilimo ili ilete Mapinduzi kwani ikifanikiwa hata pato la mwananchi na nchi litaongezeka kwani uchumi unategemea kilimo.
Alisema kuwa kilimo ni kila kitu endapo kila mhusika atatumia ujuzi na maarifa yake ambapo serikali kwa upande wake tayari imeshawezesha kwa masuala ya bajeti na wataalamu kwa kuwapatia vitendea kazi.
Alibainisha kuwa kilimo ni Sayansi hivyo watafiti wana nafasi kubwa ya kutumia Sayansi hiyo ili kuboresha kilimo ambacho kwa sasa ndiyo sekta yenye manufaa makubwa ukilinganisha na sekta nyingine.
Naye mwakilishi wa Mtendaji mkuu wa TARI Dk Juliana Mwakasendo alisema kuwa kupitia vituo vyake wanaendelea kutoa elimu kwa wakulima kutokana na tafiti zinazofanyika.
Mwakasendo alisema kuwa kwa sasa wanaondokana na dhana kuwa tafiti zinafungiwa kwani wanazisambaza ikiwa ni pamoja na teknolojia kwa njia mbalimbali ikiwa ni pamoja na siku kama hizo.
Kwa upande wake Meneja wa TARI Kibaha Hildelitha Msita alisema kuwa maadhimisho hayo yalifanyika kwenye kituo hicho kwa kuwapatia mafunzo mbalimbali wakulima kutoka kwenye baadhi ya Halmashauri za mkoa huo.
0 Comments