KAMATI ya amani ya viongozi wa dini mkoa wa Mwanza imempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa aliyoifanya ya kulitangaza taifa, kukuza uchumi na uwekezaji na kufungua fursa mbalimbali.
Akisoma pongezi la kamati hiyo leo jijini Mwanza katika mkutano wa kamati hiyo na vyombo vya habari, Mwenyekiti wa kamati, Askofu Charles Sekelwa amesema mbali na pongezi wanamshukuru na kumtia moyo aweze kuwa na hamasa ya kuendelea kufanya vizuri.
Ametaja baadhi ya mambo ambayo yamefanywa na Rais Samia na kuwasukuma kutoa pongezi hizo kuwa ni kasi ya ukuaji katika uwekezaji na uchumi, uongozi rafiki kwa vyombo vya habari, kupandisha viwango vya mishahara, kukamilisha ujenzi wa daraja la Tanzanite, kufuta stakabadhi ghalani kwa mazao ya Dengu, Choroko na Mbaazi na kupandisha bei, kupanua bajeti ya miundombinu na kuboresha barabara nchini, kuongeza ushirikiano wa sekta binafsi na serikali na kulipa madeni yakiwemo ya wakandarasi.
"Tunampongeza yeye binafsi na serikali anayoiongoza tumeona mazingira ya kisiasa ya nchi yetu yameimarika amefanya mazungumzo na viongozi mbalimbali wa kisiasa akiwemo Tundu Lissu na Freeman Mbowe," amesema Askofu Sekelwa na kuongeza
"Awali ni kama watu walikuwa wamekata tamaa kwa sababu mazingira yalijenga uadui tunapongeza hatua zinazopigwa hadi sasa, wanasiasa wote wakiwemo wa upinzani ni Watanzania, Rais aendelee kuboresha mazingira rafiki ya ufanyaji siasa nchini," amesema Askofu Sekelwa.
Katibu wa kamati hiyo, Sheikh Hassan Kabeke amesema kwa kipindi cha mwaka mmoja wa uongozi wa Rais Samia amesimamia amani na utulivu wa nchi na kudhibiri taharuki huku akiupa kipaumbele mkoa wa Mwanza katika miradi mbalimbali ya kimkakati ikiwemo stendi za mabasi za Nyegezi na Nyamhongolo, soko la kisasa la Mwanza, ujenzi meli ya MV. Mwanza na daraja la Kigongo- Busisi.
"Watu wa Kanda ya Ziwa tulipata hofu baada ya kifo cha Hayati John Magufuli juu ya hatma ya miradi hiyo lakini tunampongeza Rais Samia mambo yanakwenda vizuri wito wetu kwa Watanzania ni kuendelea kumuunga mkono," amesema Sheikh Kabeke.
Mwisho
0 Comments