Na Mwandishi Wetu_ BUKOBA.
KIJANA Victor Mwesiga (35) mkazi wa eneo la Kisindi katika kata Kashai manispaa ya Bukoba mkoani Kagera, anaomba wananchi na wadau mbalimbali wanaotoa huduma kwa watu wenye ulemavu, kumsaidia kupata matibabu na mahitaji yake ya kila siku, baada ya kupoteza uwezo wake wa kujitegemea kimaisha kutokana na kupata ajali iliyomsababishia ulemavu wa kudumu.
Akizungumzia ajali hiyo amesema akiwa Dar-es- Salaam aligongwa na gari wakati akitoa kufanya shughuli zake za ujasiriamali Julai 23, 2011 na kupelekwa katika hospitali ya Amana na baadae kuhamishiwa hospitali ya taifa Muhimbili, kwa matibabu zaidi, lakini hakupona hadi leo amekuwa mtu wa kukaa eneo moja na kulala muda wote.
"Nilipohamishiwa hospitali ya Muhimbili mwanzoni walisema watanifanyika upasuaji katika magogo wangu lakini sikufanyiwa, nilikaa hospitalini zaidi ya miezi miwili na baadae kuruhusiwa nikiwa bado sina dalili zozote za kupona" amesema.
Amesema aliporuhusiwa alipangiwa kuwa anakwenda kliniki kwa ajili ya kufanya mazoezi, lakini alishindwa maana kwa kuwa alikuwa hawezi hata kukaa, na ili aende kliniki mpaka awe na uwezo wa kukodisha gari la kumpeleka akiwa amelala, uwezo ambao hakuwa nao.
"Nilipata watu waliojitokeza kwamba wanaweza kuunga mifupa kwa kutumia tiba asili, walinisaidia kuniunga mgogo kwa sababu mwanzoni wakati naruhusiwa kutoka hospitali nilikuwa siwezi hata kuinuka, mgongo ulikuwa umeachia na ulikuwa kama unacheza, baada miezi miwili nikawa na uwezo wa kujiinua na maumivu yakawa yamepungua kidogo" amesema.
Mwesiga amesema alihisi ganzi kuanzia kiunoni kwenda mpaka miguuni na hakuweza kuchezesha hata vidole, akaelekezwa jinsi ya kufanya mazoezi, akafanya mazoezi hayo kwa muda mrefu lakini haikumsaidia, hali iliyosababisha aombe msaada kupitia redio moja, ambapo wananchi walimchangia fedha akapata nauli ya kumsafirisha kurudi nyumbani Bukoba.
Kijana huyo ambaye ni mzaliwa wa kijiji cha Rushaka kata Buhendangabo tarafa ya Bugabo, katika halmashauri ya wilaya ya Bukoba, alirejea Bukoba mwaka 2016 na sasa anaishi na dada yake katika eneo la Kisindi kata Kashai, amesema anashindwa kupata mahitaji ya kila siku kutokana na ndugu yake anayemtegemea kutokuwa na kazi ya uhakika ya kumwingizia kipato.
"Dada yangu ninayemtegemea hana kazi maalumu, naye ameolewa anamtegemea mume wake, lakini na mume wake sasa ana muda mrefu anaumwa kwa hiyo imekuwa vigumu kutuhudumia, naomba wananchi wanisaidie kwa chochote watakachowezeshwa" amesema.
Akimzungumzia kijana huyo diwani wa kata Kashai Ramadhan Kambuga, amewaasa wananchi kujitokeza kumsaidia kadri watakavyowezeshwa na Mwenyezi Mungu, ili apate mahitaji yake ya kila siku lakini na matibabu pia, maana naye hakutegemea kuishi maisha anayoishi hivi sasa ya kuwa tegemezi.
"Victoro alikuwa mtu mzima akapata ajali na kumsababishia matatizo aliyonayo sasa, hivyo anahitaji msaada wa jamii, na sio kwa Victor tu, wapo wananchi wengi wahitaji ambao wanategemea msaada waweze kuishi, tujitoe kwa moyo kuwasaidia maana kufanya hivyo mbali na kunusuru maisha yao, pia tutapata thawabu kutoka kwa Mwenyezi Mungu" amesema diwani huyo.
Kwa mujibu wa kijana huyo wakati anapata ajali alikuwa na mke na mtoto mmoja, lakini baada ya ajali mke aliondoka na kumwacha peke yake na mtoto wake kuchukuliwa na hadi sasa hafahamu ni vipi atapata mtoto wake.
0 Comments