NA AMON MTEGA,_ SONGEA.
WAZIRI wa Habari Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Nape Nnauye amewaomba Viongozi wa dini Nchini kuwahamasisha Watanzania kushiriki kikamilifu zoezi la Anwani za makazi na Postikodi ili liweze kukamilika kwa wakati.
Nape ametoa ombi hilo Mkoani Ruvuma wakati akiangalia zoezi la Anwani za makazi na Postikodi linaloendelea Nchi nzima kwa lengo la kuboresha makazi ya Wananchi ili kuendana na mfumo wa kisasa.
Akizungumza Mkoani humo amesema kuwa zoezi hilo ni la muhimu hivyo kila mmoja anatakiwa kushiriki kikamilifu ikiwemo Viongozi wa dini kuwahamasisha waumini wao wanaongoza.
"Nawaombeni Viongozi wangu wa dini tusaidiane kulitekeleza jambo hili la Anwani za makazi na Postikodi ili Wananchi wetu wawe na makazi bora ya nayoendana na mfumo wa Dunia wa sasa "amesema Waziri Nape Nnauye.
Waziri Nape licha ya kutoa ombi hilo kwa Viongozi wa dini amesema kuwa makazi ambayo yapo kwenye maeneo ya migogoro ikiwemo waliojenga mabondeni hawatahusishwa na zoezi hilo mpaka pale migogoro yao itakapopatiwa ufumbuzi.
Amefafanua kuwa kwa wale ambao makazi yao yamekuwa na migogoro licha ya kutokushiriki zoezi la Anwani za makazi na Postikodi watashiriki zoezi la kuhesabiwa Sensa ili kujua takwimu halisi ya Wananchi.
Aidha Waziri Nape ameupongeza Mkoa wa Ruvuma kufuatia zoezi la Anwani za za makazi na Postikodi kuwa limefanyika vizuri kufuatia kaya nyingi kufikiwa na zoezi hilo ambalo kwa mkoa huo litakamilika Aprili 30 mwaka huu.
Hata hivyo Nape amewataka Mamlaka ya barabara za Mjini na Vijijini (Tarura)kuziangalia barabara za kwenye mitaa kuzipatia majina ya watu ambao walifanya kazi kwenye jamii ili kujenga Historia kwa vizazi vijavyo.
Kwa upande wake mkuu wa mkoa wa Ruvuma Balozi Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge amesema kuwa mkoa huo umejipanga vema hadi sasa umekuwa mkoa wa kumi kitaifa katika kufanikisha zoezi hilo ambapo sawa na asilimia 97.62.
0 Comments