Na Fatma Ally Matukio Daima APP, Dar es Salaam
Chama cha Maafisa Uhusiano kwa Umma Tanzania kinatarajia kufanya Mkutano wa Maafisa Habari wa Afrika kwa mwaka 2022 ambapo pamoja na mambo mengine umelenga kuitangaza Tanzania katika nyanja mbalimbali ikiwemo Utalii.
Akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dar es Salaam, Katibu Mkuu wa Chama Cha PRST Ndege Makura amesema mkutano huo utahusisha matukio makubwa 4 ikiwemo kuwakutanisha wanafunzi wa vyuo wanaosoma Taaluma ya Mahusiano kwa umma kubadilishana uzoefu pamoja na kutangaza utalii wa Tanzania.
Aidha amesema mkutano huo ni wa 33 lakini unafanyika kwa mara ya kwanza Tanzania ambapo hadi sasa nchi 23 zimedhibitisha kushiriki kwa upande wa Afrika na nje ya Afrika ambapo amesema waandishi na maafisa ndio watu wa kwanza wa kuisemea Afrika kwa mazuri.
"Mkutano huo utafanyika kuanzia tarehe 23 mpaka 27 mwezi Mei katika ukumbi wa Mwalim Julius Nyerere, mpaka sasa watu wanaendelea kujiandikisha, tunategemea tutapokea idadi kubwa zaidi ya wageni, niwaombe wadau wa habari washiriki Mkutano huu ambao umelenga kuisemea Afrika katika mambo mazuri "amesema Ndege.
Kwa upande wake, Makamo wa Rais PRST Mary Kafyome amesema mpaka sasa wageni zaidi ya 300 wamethibitisha kushiriki katika Mkutano huo maalum ambao unakwenda kutoa matokeo chanya kwa nchi ya Tanzania.
Aidha amewataka wadau wa habari wakiwepo maafisa habari wa vyama mbalimbali kushiriki katika Mkutano huo Ili waweze kujiongezea maarifa katika taaluma zao, kwani wataweza kujifunza mambo mbalimbali.
Naye, Kaimu Mwenyekiti wa Bodi PRST Jossey Makasyuka amesema miongoni mwa wageni watakaokuwepo ni pamoja na viongozi wakuu wa Serikali, Rais wa chama cha PR Afrika pamoja na Rais wa Benki ya Maendeleo Afrika na Mkurugenzi wa Airtel Afrika.
Aidha amesema wanatarajia kujifunza na kubadilishana uzoefu katika taaluma hiyo na utatoa dira na mstakabali wa Afrika katika kuitangaza kwa mtazamo chanya.
0 Comments