Header Ads Widget

TAASISI NA WATU BINAFSI BIHARAMULO WAOMBWA KUSAIDIA JAMII

Na Matukio Daima APP Biharamulo

TAASISI mbalimbali na watu binafsi wenye uwezo kiuchumi wameaswa kutumia sehemu ya kipato chao  kutoa misaada kwa watu wenye uhitaji, ili kuwapunguzia changamoto za ugumu wa maisha zinazowakabili.


Kauli hiyo imetolewa na sheikh wa wilaya ya Biharamulo Hamza Khatib Hamza, wakati akipokea swadaka ya futari kutoka kwa mbunge wa jimbo la Biharamulo Magharibi mhandisi Ezra Chiwelesa.


Sheikh Hamza amesema kuwa futari hiyo wataigawa kwa wahitaji kwa uadilifu mkubwa, ili kuhakikisha inawafikia walengwa.


Ametumia fursa hiyo kumshukuru Chiwelesa, kwa utaratibu huo aliojiwekea kila mwaka tangu amekuwa mbunge, ambapo amekuwa akitoa futari kwa ajili ya wahitaji kila unapofika mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhan, na kuwa mbunge huyo ni mfano wa kuigwa na watu wote wenye uwezo kiuchumi.


Akikabidhi futari hiyo kwa niaba ya mbunge huyo, mwakilishi wake ambaye pia ni diwani wa viti maalumu Ziyuni Hussein amesema kuwa futari hiyo imetolewa na mbunge kwa lengo la kuwafuturisha Waislamu wote wa Wilaya ya Biharamulo ambao uongozi wa dini hiyo utaona wanastahili kupata.


Hussein ametaja baadhi ya vitu vilivyotolewa na mbunge huyo kuwa ni tende boksi 25, ndoo 25 za mafuta ya kula zenye ujazo wa lita kumi, mchele mifuko 25 yenye uzito wa kilo 25 kila mfuko, unga wa sembe mifuko 25 yenye uzito wa kilo 25 kila mfuko , unga wa ngano mifuko 25 yenye uzito wa kilo 25 kila mfuko na Maharage mifuko 25 ambayo kila mfuko una uzito wa kilo kumi.


Amesema mbunge huyo  anaungana na waumini wote wa dini ya Kiislamu katika mfungo huo, licha ya kuwa yupo Bungeni akiendelea na majukumu ya kuwawakilisha wananchi wake.


Naye Sheikh wa kata ya Biharamulo mjini Abdul-hafidh  Rashid akizungumza kwa niaba ya Masheikh wa kata na waumini wa dini hiyo,  amemshukuru mbunge huyo na kwamba wao kama viongozi wanaoishi na waumini huko mitaani, wanatambua kuwa wanaohitaji ni wengi, na kuongeza kuwa swadaka hiyo itawasaidia kupunguza makali ya maisha katika mfungo huu hasa kwa siku zilizobakia.


Rashid amesema kuwa watahakikisha wanawapatia wale ambao wana mahitaji na kwamba pia wataigawa swadaka hiyo kwa uadilifu mkubwa, huku wakitegemea Radhi za Allah Subuhana Wataala.



Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI