Header Ads Widget

SOS KUENDESHA MAFUNZO YA MALEZI BORA KWA WATOTO



Mratibu Mkuu wa Malezi mbadala wa Taasisi isiyokuwa ya kiserikali ya SOS Tanzania, Onesmo Itozya (katikati) akielezea umuhimu wa mafunzo ya malezi kwa watoto wanaolelewa kwenye makao ya taasisi hiyo jijini Dar es Salaam leo April 11, 2022.

NA ARODIA PETER MATUKIO DAIMA APP

DAR ES SALAAM

TAASISI isiyokuwa ya kiserikali ya SOS Village imeanza program maalum ya kuwajengea uwezo wakuu wa kaya wa Kijiji chake kuhusu malezi ya watoto.


Wakuu hao wa kaya ni wanawake 13 wanaotunza watoto 118 waliopoteza malezi ya familia zao halisi na wengine wanatoka kwenye mazingira magumu.


Akitoa maelezo kwenye uzinduzi wa mafunzo hayo leo April 11, 2022 Jijini Dar es Salaam, Mratibu Mkuu wa Malezi mbadala wa SOS Tanzania Bara na Zanzibar, Onesmo Itozya amesema wamelazimika kutoa mafunzo hayo ili kukidhi kanuni za makao hayo ambayo yanawataka walezi wa watoto walio kwenye vituo vyao kuwa na ujuzi wa malezi kuanzia ngazi ya cheti.


Amesema ili kuendana na hali ya sasa watoto wanahitaji kukaa na watu wenye uelewa juu ya masuala ya malezi na saikolojia ambayo inabeba mabadiliko ya tabia na makuzi yao kwa ujumla. 


Amesema mafunzo hayo yatakayojumuisha wanawake walezi 13 yatatolewa na wakufunzi wabobezi kutoka Chuo cha Ustawi wa Jamii cha Kisanga kilichopo mkoani Kilimanjaro kwa miezi minane.


"Tanzania kwa sasa ina uhitaji wa malezi ya kitaalam, hivyo lazima wataalam hao waandaliwe ili kukabiliana na changamoto nyingi za malezi na makuzi ya watoto. 


"Kama mnavyofahamu vituo vyetu vinapokea watoto wenye umri na tabia tofauti, hivyo wanahitaji kulelewa katika misingi ya kifamilia lakini kwa kutumia watu wenye taaluma ya malezi." amesema  Itozya. 


Kwa upande wake, Naibu Mkuu wa Taasisi ya Ustawi wa Jamii, Utafiti, Mafunzo na Ushauri wa Kitaalam, Profesa  Satco Komba amesema changamoto kubwa zinazosababisha watoto wa mitaani kuongezeka zinachangiwa na kutetereka kwa ndoa na kutengana kwa wazazi. 


Amesema changamoto hiyo imesababisha jukumu la kulea watoto kutetereka na   watoto kukosa mwelekeo na hivyo kupoteza ndoto zao za maisha.


"Program za SOS zinatengeneza kizazi na kukuza taasisi ya familia.  Kwa mfano haya mafunzo yaliyozinduliwa leo yatawapatia hawa akina mama ambao ni walezi wa hawa watoto kupata ujuzi mwingi ukiwemo wa malezi,  namna ya kutatua changamoto za kisaikolojia pamoja na suala zima la Ulinzi na usalama ambalo limekuwa tishio kwa watoto katika miaka ya karibuni" amesema Profesa Komba. 


Mmoja wa akina mama wanaotarajia kupata mafunzo hayo, Bi Theresia Shayo ameshukuru program hiyo kwani  wanatarajia kupata ujuzi na mbinu mpya za kitaalamu kuhusu malezi ya watoto kwa ujumla wake.


Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI