NA WILLIUM PAUL, MOSHI.
MADIWANI wa Halmashauri ya Manispaa ya Moshi mkoani Kilimanjaro wamemuondoa katika nafasi yake Mstahiki Meya wa manispaa hiyo, Juma Rahibu baada ya kupa kura za kutokuwa na imani naye katika mkutano maalum wa Baraza.
Miongoni mwa sababu zilizopelekea Mstahiki Meya huyo kuondolewa na Madiwani hao nia pamoja na tuhuma za kushiriki sherehe ya kuzaliwa kwa kijana anayetuhumiwa kushiriki mapenzi ya jinsia moja (shoga), pamoja na kutumia nafasi yake vibaya.
Akitoa taarifa katika Baraza hilo, Mkurugenzi wa halmashauri ya manispaa ya Moshi, Rashid Gembe alisema kuwa, awali ofisi yake ilipokea barua kutoka kwa Madiwani 20 kati ya 30 wa halmashauri hiyo mnamo Machi 17 wakitaka kuitishwa mkutano maalum wa kumuondoa Mstahiki Meya.
Mkurugenzi huyo alisema kuwa, alimtaarifu Mstahiki Meya huyo tuhuma na sababu za kutaka kuondolewa madarakani na kumtaka kuandaa majibu ya tuhuma hizo ndani ya siku tano baada ya kupokea tuhuma.
Alisema kuwa, Meya Juma Rahibu aliwasilsha majibu ya utetezi ambapo kanuni ya 5 kifungu kidogo 4 za halmashauri inamwelekea Mkurugenzi kuwasilisha tuhuma na majibu ya Meya kwa mkuu wa mkoa ambapo alifanya hivyo.
Aliendelea kudai kuwa, kuwa kanuni ya 5 kifungu kidogo 5 kinampa mamlaka Mkuu wa Mkoa kuunda timu ya uchunguzi ambapo alifanya hivyo na timu hiyo ilitekeleza majukumu yake kama ilivyoelekezwa ambapo Mkuu huyo wa mkoa aliwasilisha uchunguzi wa timu hiyo kwa Mkurugenzi wa halmashauri.
Akisoma taarifa ya timu hiyo iliyoundwa na Mkuu wa mkoa mbele ya baraza alisema kuwa, moja ya vitu ilivyokuwa ikichunguza ni pamoja na kubaini kama Mstahiki Meya anatumia nafasi yake vibaya na kutoa maamuzi ambayo hayajapitishwa na baraza la Madiwani na kutowaheshimu viongozi wanaohudhuria vikao, mikutano ya halmashauri.
Jambo jingine ni kuchunguza na kubaini kama Mstahiki Meya ameshiriki katika vitendo vya rushwa hususani katika usimamizi wa ujenzi holela kwenye eneo la katikati ya mji (CBD), manispaa ya Moshi.
Timu hiyo pia ilichunguza na kubaini kuwa Mstahiki Meya anamwenendo mbaya au ukosefu wa adabu dhidi ya Waheshimu Madiwani anaowaongoza.
Nne ni kuchunguza tabia na mwenendo wa Mstahiki Meya katika jamii kwa kuhusisha nafasi na wadhifa wake kutokana na tuhuma zilizotolewa na wananchi na baadhi ya vyombo vya habari kuwa Meya alishiriki sherehe za kuzaliwa mmoja wapo wa kijana anayejihusisha na mahusiano (mapenzi) ya jinsia moja (ushoga) na kulishwa keki na watu wa jamii hiyo.
Katika majibu ya uchungu wa kamati hiyo ya Mkuu wa Mkoa ilibaini yapo baadhi ya maeneo ambayo Mstahiki Meya anatuhumiwa kutumia madaraka yake vibaya na kutowaheshimu viongozi waliohudhuria vikao kama tuhuma zinavyoonyeshwa kukiuka mwongozo wa mwaka 2016 uliotolewa na ofisi ya Rais Tamisemi.
Mwongozo huo unaelekeza kuwa wajumbe waliochaguliwa kwenye kamati mbalimbali baada ya uchaguzi mkuu watakaa madarakani kwa muda wa miezi 18 ndipo uchaguzi mwingine ufanyike hata hivyo katika halmashauri ya manispaa ya Moshi Wajumbe hao walikaa madarakani kwa kipindi cha miezi 7 tu.
Kutoruhusu mjadala katika kamati ya fedha na utawala ambacho kilitakiwa kujadili swala la vikundi vilivyoomba na kupatiwa mikopo.
Kwenye tuhuma za kubadili maamuzi ya kutoa fedha za ujenzi wa jengo la mama na mtoto katika kata ya Kaloleni, miuktasari haionyeshi mahali ambapo halmashauri iliridhia kuhamisha matumizi ya fedha za ujenzi wa jengo la mama na mtoto kutoka zahanati ya Kaloleni kwenda kujenga kichomea taka katika kituo cha Afya Pasua kilichopo kata ya Bomambuzi.
Timu hiyo ya uchunguzi ilithibitisha Mstahiki Meya kutumia madaraka yake vibaya.
Taarifa hiyo hiyo ya timu ya uchunguzi iliendelea kubainisha kuwa, kutokana na majibu ya wahojio wa tume hiyo baadhi ya wajumbe walieleza kuwa Mstahiki Meyaanahusika na kupokea rushwa ili kuruhusu ujenzi katika maeneo ya katikati ya mji nay eye mwenyewe kukiri hivyo katika kikao cha kamati ya siasi ya wilaya.
Timu ya uchunguzi haikubaini utthibitisho wa jambo hilo pamoja na kwamba kunaviashiria vya rushwa katika kutoa vibali vya ujenzi.
Akiendelea kusoma taarifa hiyo, Mkurugenzi Gembe alisema kuwa, yapo mambo yanayofanywa na Mstahiki Meya yanayoonyesha kuwa anamwenendo mbaya na ukosefu wa adabu dhidi ya Madiwani anaowaongoza ikiwa ni pamoja na kutoa kauli ya kuwatambia madiwani wenzake kwamba yeyeMeya ni mteule wa kamati kuu ya CCM Taifa na kwamba hakupendekezwa na ccm wilaya wala mkoa katika nafasi ya Umeya.
Ametajwa mara nyingi akiwaita Madiwani wenzake hawajui kitu mara kwa mara huchelewa kwenye vikao kabla ya baraza na akifika haombi radhi wenzake kwa kuchelewa pamoja na kutomkaimisha ofisi Naibu Meya na kutomruhusu kuendesha vikao kwa niaba yake anapokuwa nje ya ofisi.
Alisema kuwa, kunawakati haruhusu mijadala kwenye vikao na mikutano ya halmashauri pamoja na kutoa kauli zisizo na staa kwa Madiwani wenzake hivyo timu ya uchunguzi imedhibitisha kuwa Mstahiki Meya anamwenendo mbaya na kuwakosea adabu Madiwani wenzake.
Kuhusu swala la sherehe, timu imebaini kuwa Mstahiki Meya alishiriki katika sherehe ya kuzaliwa kijanaanayetuhumiwa kujihusisha na mahusiano ya mapenzi ya jinsia moja (Ushoga), nay eye mwenyewe alikiri kushiriki kwa utetezi kwamba mwaliko huo uliletwa kwake kama Juma Rahibu na sio kama Meya.
Aliendelea kudai kuwa, wala hakwenda kushiriki sherehe hizo kwa mamlaka aliyonayo kwani hakutumia gari la halmashauri wala kuvaa mkufu wa mamlaka ya Umeya na katika utetezi wake wa maandishi alieleza kuwa swala hilo kuendelea kujadili linachochea ubaguzi dhidi ya makundi flani katika jamii na kutaka kuharibu tunu ya Taifa uhuru na Umoja.
Timu ya uchunguzi imethibitisha kwamba Mstahiki Meya alishiriki katika sherehe husika na tukio hilo halionyeshi taswira nzuri kwa jamii anayoiongoza na ni kinyume cha maadili ya Madiwani, utamaduni, mila na desturi za nchi.
Akitoa matokeo ya kura, Mkurugenzi wa manispaa ya Moshi, Rashidi Gembe alisema kuwa, Madiwani waliopiga kura ni 28 ambapo kura 18 ziliridhia kuondolewa kwa Mstahiki Meya Juma Rahibu huku kura 10 zikitaka Mstahiki Meya huyo kuendelea katika nafasi yake.
Kutokana na matokeo hayo, Mstahiki Meya Juma Rahibu ameondolewa madarakani ambapo nafasi yake itakaimishwa kwa Naibu Meya, Stauti kwa kipindi chote cha mpito hadi atakapochaguliwa Mstahiki Meya mwingine aidha kwa mujibu wa kanuni ya 5 kifungu kidogo 8 endapo Meya hataridhika na uamuzi wa baraza atakata rufaa kwa Waziri wa Tamisemi kuhusu utaratibu uliotumika kumuondoa madarakani.
Mwisho…..
0 Comments