Header Ads Widget

HALI TETE KWA WAMILIKI MAJENGO MJI WA MOSHI

 


Na  Gift Mongi,Matukio Daima APP,

Moshi

Hali sii nzuri kwa wamiliki wa majengo yaliyojengwa kwa siku za hivi karibuni katikati ya manispaa ya Moshi bila kufuata utaratibu na sheria za kuendeleza eneo la kibiashara mjini (CBD)kwani wengi wao wametajwa kujipatia vibali kwa njia zisizo rasmi ikihusisha vitendo vya rushwa.


Ujenzi wa nyumba hizo ambazo zimeoteshwa mithili ya uyoga umebainika kufanyika zaidi katika kata za Bondeni na Mawenzi ambazo zipo katikati ya manspaa ya Moshi ambapo ujenzi wake ulikuwa ukifanyika kwa nyakati za usiku,mwisho wa wiki au wakati wa sikukuu.


Vibali vya ujenzi wa nyumba hizo vilikuwa vikiidhinishwa na aliyekuwa  meya wa manispaa ya Moshi Juma Rahibu ambapo tayari alishang'olewa katika wadhfa wake huo na tuhuma nyingine ambazo amezikiri ni kupokea kiasi cha fedha kwa wenye majengo hayo kati ya milioni 2 hadi 3 kulingana na ukubwa wa nyumba ulivyo.


Kwa muktadha huo taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa(TAKUKURU)haitakuwa na majukumu mazito katika uchunguzi dhidi ya vitendo vya rushwa kwani tayari upande mmoja(mpokeaji)ameshakiri kujihusisha na matukio hayo yote.


Mkuu wa taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa(TAKUKURU) mkoa wa Kilimanjaro Frida Wikes alikaririwa akisema kuwa uchunguzi juu ya(Juma)ulishaanza na kuwa tuhuma Ni nyingi lakini pia ni mapema mno kuzungumzia suala hilo.


'Tuhuma za aliyekuwa meya(Juma)tumezipokea na uchunguzi unaendelea na ni ngapi siwezi kusema maana ni nyingi lakini ni vyema ukanipa muda ili tukamilishe taratibu zetu kwanza"alisema


Jaffary Michael ni meya mstaafu wa manspaa ya Moshi ambapo  alisema wakati wa utawala wake alijitahidi sana kusimamia sheria na kuepusha ujenzi holela lakini kwa sasa imekuwa tofauti kwani mazingira ya usimamizi wa utoaji vibali ulighubikwa na rushwa na hatimaye sheria kuvunjwa na msimamizi mwenyewe.


Malengo ni Moshi kuwa jiji lakini ili kufikia huko ni lazima tuujenge mji wetu ndipo tukahamua sasa tuujenge kwenda juu yaani ghorofa lakini sasa  kwa kuwa kuna kikundi cha watu wachache waliona ni fursa ya upigaji basi mambo ndio kama haya unayoyaona sasa hapa katikati ya mji yaani tunarudi nyuma badala ya kwenda mbele.


Akisoma mapendekezo yaliyotolelewa na kamati iliyoundwa na mkuu wa mkoa kumchunguza Juma Rahibu mkurugenzi wa manspaa ya Moshi Rashid Gembe alisema timu hiyo ya uchunguzi ilithibitisha aliyekuwa mstahiki meya kutumia madaraka yake vibaya.


Taarifa hiyo hiyo ya timu ya uchunguzi iliendelea kubainisha kuwa, kutokana na majibu ya wahojiono na tume hiyo baadhi ya wajumbe walieleza kuwa Mstahiki Meya(Juma) anahusika na kupokea rushwa ili kuruhusu ujenzi katika maeneo ya katikati ya mji na yeye mwenyewe kukiri hivyo katika kikao cha kamati ya siasa ya wilaya.


Akiendelea kusoma taarifa hiyo, Mkurugenzi Gembe alisema kuwa, yapo mambo yaliyofanywa na Mstahiki Meya(Juma) yanayoonyesha kuwa anamwenendo mbaya na ukosefu wa adabu dhidi ya madiwani aliokuwa anawaongoza ikiwa ni pamoja na kutoa kauli ya kuwatambia madiwani wenzake kwamba yeye Meya ni mteule wa kamati kuu ya CCM Taifa na kwamba hakupendekezwa na ccm wilaya wala mkoa katika nafasi ya umeya.


Mwisho

Post a Comment

1 Comments



MAGAZETI



BBC NEWS