Header Ads Widget

RC KUNENGE ATANGAZA KIAMA KWA WAKULIMA WALIOSHINDWA KUSAFISHA MASHAMBA YAO YA KOROSHO

 


MKUU wa Mkoa wa Pwani Abubakari Kunenge amesema kuwa watatumia sheria ndogo kuwanyang'anya mashamba wakulima wa zao la Korosho wanaoshindwa kusafisha mashamba yao.


Aidha amesema baadhi ya wananchi wamekuwa wakilalamikia wawekezaji wakubwa ambao hawaendelezi mashamba na kutaka wanyanganywe na wapewe wao.


Kunenge aliyasema hayo Mlandizi Wilayani Kibaha wakati wa uzinduzi zoezi la upaliliaji mikorosho na kuwa sheria hizo ni kutaka wakulima kusafisha mashamba yao.


Alisema kuwa baadhi ya wakulima wa zao la korosho wamekuwa hawasafishi mashamba yao na kusababisha kupata mazao hafifu licha ya kuwa zao hilo ni zao la kibiashara.


"Tutatumia sheria ndogo ndogo kuwadhibiti wakulima ambao hawasafishi mashamba yao au kutopulizia dawa kwani malengo ni kuhakikisha korosho za mkoa wa Pwani zinakuwa na ubora na kuongeza kipato cha wakulima,"alisema Kunenge.


Alisema kuwa pembejeo za zao la korosho zitatolewa kwa wakulima ambao watakuwa wameandaa vizuri mashamba yao na kwa wale ambao hawasafishi mashambao yao hawatapewa pembejeo.


"Uchumi wa mkoa wa Pwani unategemea sana zao la korosho hivyo tutahakikisha tunatumia njia zote ili Pwani iwe moja ya mikoa inayozalisha korosho nyingi na zenye ubora kama ilivyo kwa mikoa ya Kusini,"alisema Kunenge.


Kwa upande wake kaimu Mkurugenzi wa Mkuu wa Bodi ya Korosho Tanzania (CBT) Francis Alfred alisema kuwa watatoa bure lita 780,000 ambapo sulpher mahitaji ni tani 35.


Alfred alisema kuwa mahitaji ya sulpher ni tani 25 na viuatilifu vya maji ni milioni 1.5 na viuatilifu vya maji vilivyopo ni 800,000 na sulpher ni 1,600 na hadi mwezi ujao utafika 7,500 hadi 8,000 na kuanza kugawiwa kwa wakulima.


Naye mwenyekiti wa Chama Kikuu cha Ushirika Mkoa wa Pwani (CORECU) Musa Mng'eresa alisema kuwa wanaipongeza serikali kwa kufanya bei ya korosho kulipwa kutokana na ubora wake.


Mng'eresa alisema kuwa watatoa mifumo 200 ya sulpher kwa wakulima na mabomba watawalipia nusu wakulima na wao watalipa nusu na kuwa wilaya za Mkuranga na Rufiji kuna maeneo yanatoa korosho zenye ubora kuliko hata zile zinazolimwa Kusini mwa Afrika.


Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



BBC NEWS