NA AMON MTEGA,MATUKIO DAIMA APP RUVUMA
MEYA wa Manispaa ya Songea Mkoani Ruvuma Michael Mbano amewataka Wazazi na Walezi ambao wanawatoto wanaosoma kuanza kuchangia chakula kwenye shule wanazosoma watoto hao ili kupunguza utoro unaosababishwa na njaa.
Wito huo ameutoa wakati akitoa taarifa ya utekelezaji wa miradi mbalimbali inayofanywa ndani ya Manispaa hiyo katika kipindi cha Serikali ya awamu ya sita inayoongonzwa na Rais Samia Suluhu Hassan.
Mbano akitoa taarifa hiyo kwenye sekta ya Elimu mbele ya waandishi wa Habari wa Mkoa wa Ruvuma amesema kuwa kumekuwepo na baadhi ya wazazi na Walezi kujiona kama hawana wajibu wa kuchangia huduma (Chakula) kwa watoto wao wanaosoma kwa madai kuwa mzigo wote ni waserikali jambo ambalo hurudisha nyuma maendeleo ya Elimu .
Meya huyo amesema kuwa Serikali imeweka mazingira ya mwanafunzi kusoma elimu pasipo malipo toka ngazi ya Awali hadi Sekondari kidato cha Nne hivyo wajibu wa mzazi na Walezi ni kuhakikisha wanafunzi hao wanapatiwa huduma za sare ,madaftari pamoja na chakula .
Aidha Meya huyo alizipongeza shule hasa za Sekondari ikiwemo Sekondari ya Mletele kuwa walianza utaratibu wa wanafunzi kula chakula shuleni mapema jambo ambalo limeonyesha kuwa na mafanikio ya kupunguza utoro kwenye shule hizo.
Hata hivyo Mbano ameipongeza Serikali ya awamu ya sita inayoongonzwa na Rais Samia Suluhu Hassan pamoja na mbunge wa jimbo la Songea mjini Dkt Damas Ndumbaro ambaye pia ni Waziri wa Maliasili na Utalii kuwa wameboresha miundombinu ya shule ambayo imewafanya wanafunzi kuzipenda shule hizo kisha kusoma kwa bidii.
0 Comments