NA WILLIUM PAUL, MOSHI.
MBUNGE wa jimbo la Moshi vijijini mkoani Kilimanjaro, Prof. Patrick Ndakidemi, amefanya ziara ya kutembelea wakulima wawili wajasiriamali wa kilimo katika kata mbili za Kindi na Kibosho Kirima lengo likiwa ni kukuza uchumi.
Mbunge huyo amewatembelea vijana hao machachari wanaojishughulisha na kulima mbogamboga na kuzipeleka masokoni.
Aidha Mbunge huyo aliwatembelea vijana mapacha Kurwa na Doto Ahmed Mushi wa kijiji cha Boro kata ya Kibosho Kirima na kujionea kilimo cha mazao ya Biringanya na Ngogwe ambapo Vijana hao walimhakikishia mbunge kuwa kilimo cha mbogamboga kinalipa, na hiyo ni ajira yao ya kudumu kwani inawapatia kipato cha kutosha.
Prof. Ndakidemi akiambatana na Madiwani wa Kata ya Uru Kusini Wilihad Kitally na Kibosho Umbwe, Prosper Massawe walimtembelea kijana mwekezaji Ombeni Nyange ambaye amewekeza kikamikifu kwenye kilimo cha nyanya, ndizi, ufugaji wa Samaki, kuku, bata, mbuzi wa kisasa, sungura na bata mzinga katika kata ya Kindi.
Mjasiriamali Nyange amelima nyanya kwa kutumia mbinu bora za ukulima wa kisasa ambapo kijana huyu ametoa ajira za kitosha kwa akina mama na baba kutoka vijiji vya jirani.
Nyange alisema kuwa shamba lake huzalisha nyanya zinazopelekwa kwenye masoko mbalimbali nchini kwa kipindi cha mwaka mzima.
Wajasiriamali wote wawili walimweleza mbunge kuwa changamoto yao kubwa ni soko la uhakika huku pia wakidai kunakipindi bei za soko zinakuwa ndogo sana na kusababisha hasara.
Ombeni alimwomba mbunge amsaidie ili aanzishe kiwanda kidogo cha kusindika nyanya ambapo Mbunge huyo aliahidi kufikisha ombi lake kwenye mamlaka husika, likiwemo shirika la TAHA.
Mbunge Ndakidemi aliwashukuru vijana hao, na kuwaomba wawe mabalozi wa kilimo cha mbogamboga huku akiahidi atakuwa anapeleka vikundi vya vijana ili wakajifunze kwa vitendo kutoka kwa vijana hawa ambao wamefanikiwa.
Baada ya ziara Mbunge amewashauri vijana kujituma kama akina Ombeni, na ana matarajio makubwa ya kuona matokeo chanya ya kujipatia kipato cha uhakika na maendeleo kama watajishughulisha na kilimo.
Mwisho...
0 Comments