MRADI WA UPANUZI WA BANDARI YA TANGA WAFIKIA 26% WA UJENZI WAKE.
Teddy Kilanga
Arusha
Mradi wa uboreshaji wa bandari ya Tanga kwa awamu ya pili wa ujenzi wa gati la kwanza na pili umefikia katika asilimia 26 ambapo matarajia ya kukamilika kwake ni Oktoba ,16,2022.
Akizungumza na waandishi wa habari,Mhandisi Hamis Kipalo alisema mradi huo umefikia asilimia 26 lakini pamoja na matarajio hayo ya kukamilika kwa mradi huo Mkandarasi yupo nyuma ya muda hivyo inasadikika ataongezewa muda wa utekelezaji wa mradi huo.
"Mkandarasi yupo nyuma ya muda kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo mlipuko wa ugonjwa wa Covid -19 ambapo nchi nyingi zilifungwa na baadhi ya vifaa huagizwa nje ya nchi,"alisema Mhandisi Kipalo.
Alieleza kuwa mradi huo unaurefu wa mita 450 na upana mita 50 ambapo ulianza kutekelezwa Septemba 5,2020 ambapo utatekelezwa ndani ya miezi 22.
Alisema pamoja na mkandarasi huyo kusadikika kuongezewa muda kutokana na changamoto hizo pia atakabidhi kipande cha mradi chenye urefu wa mita 150 kati ya 450 ili kuweza kuanza kazi.
Mhandis Kipalo alisema mradi huo utaleta manufaa kwa wananchi na wafanyabiashara katika kuongeza ufanisi wa bandari kutoka tani laki saba na nusu hadi milioni tatu ambapo uwezo wa bandari utaongezeka na kufanyika haraka tofauti na mwanzoni.
"kutokana na kuongezeka kwa ufanisi wa bandari pia kutasaidia kufanyika kwa biashara katika ukanda wa kaskazini na Afrika ya mashariki hali ambayo itaongeza wateja,"alisema.
Kwa upande wake Afisa Uhusiano wa bandari ya Tanga,Adam Shindo alisema wameshiriki katika maonyesho hayo ya TANZFOOD EXPO kwa lengo la kusogea karibu na wateja katika kuwaelezea huduma wanazozitoa pamoja na kuwaelezea manufaa ya upanuzi wa bandari ya Tanga.
Mradi huo unatekelezwa na kampuni ya CHEC kutoka China na kusimamiwa na Mhandisi mshauri kutoka Denmark ikishirikiana na kampuni ya kitanzania Anova.
0 Comments