Na Editha Karlo, Kigoma
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) mkoa Kigoma kimesema kuwa hakitavulimia kuona viongozi na watendaji wake wakiingiza wageni kutoka nje ya nchi kugombea nafasi au kushiriki kwenye uchaguzi wa ndani wa chama hicho.
Katibu wa CCM mkoa Kigoma, Mobutu Malima akizungumza na madiwani na wakuu wa idara wa halmashauri ya wilaya Kakonko jana amewaonya madiwani na wenyeviti wa vijiji watakaoingiza raia wa kigeni kwa ajili ya kugombea au kushiriki kwa namna yeyote kwenye mchakato wa uchaguzi wa ndani wa viongozi wa chama hicho unaoendelea watashughulikiwa.
Malima alitoa kauli hiyo wilayani Kakonko akiongoza sekretariet ya chama hicho kujitambulisha kwenye mamlaka mbalimbali za uongozi katika wilaya za mkoa Kigoma baada ya uteuzi uliofanywa hivi karibu kwa watendaji wa chama hicho nchi nzima.
Malima alisema kuwa wilaya za mkoa Kigoma ziko mpakani na nchi jirani na kuwa na mwingiliano mkubwa wa wageni kutoka nchi hizo ikiwemo Burundi ambao wamekuwa wakiingia na kuishi nchini wengine bila kufuata taratibu na baadhi yao kujiingiza kwenye michakato ya siasa kwa kugombea nafasi mbalimbali au kupata uhalali wa kupiga kura jambo ambalo ni kinyume na taratibu za chama lakini pia sheria za nchi.
Kutokana na hali hiyo Katibu huyo wa CCM mkoa Kigoma amewataka viongozi hao kutoa ushirikiano kwa kuwaripoti kwenye vyombo vya usalama wageni wanaoingia kwenye maeneo yao.
Sambamba na hilo Katibu huyo wa CCM mkoa Kigoma amezungumzia kuwepo kwa ushirikiano baina ya madiwani nawakuu wa idara za halmashauri ili kutumiza lengo la kuwatumikia wananchi na kwamba migogoro na kuazimiana kusiko na tija kwa ajili ya maslahi binafsi kusipewe nafasi kwani ni moja ya vikwazo katika usimamizi wa kuleta maendeleo kwa wananchi.
Awali Katibu wa Jumuia ya wazazi mkoa Kigoma, Sarah Kairanyah amezitaka halamshauri za mkoa Kigoma kutoa taarifa za utekelezaji wa shughuli za kuleta maendeleo kwa wananchi kwani jambo hilo lipo kisheria ili kukiwezesha chama kusimamia utekelezaji huo katika muktadha wa usimamizi wa utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya CCM.
Kailanya alisema kuwa ni lazima taarifa hizo zinapoombwa zitolewe kwa wakati ili kuruhusu mamlaka na vikao mbalimbali vya chama kuzifanyia kazi kwa kutoa ushauri na kuchukua hatua kwenye maeneo ambayo utendaji au watendaji hawatimizi majukumu yao kwa mujibu wa taratibu.
0 Comments