Na Andrew Chale, Dar es Salaam.
WAFANYAKAZI zaidi ya 200, Waliokuwa wakifanyakazi katika kampuni ya New Habari (2006) Ltd, wametoa siku 14 kwa Mmiliki wa Kampuni hiyo, Mfanyabiashara na Bilionea Rostam Aziz awe amepeleka fedha za mafao katika mifuko ya Hifadhi ya Jamii ikiwemo NSSF na PSSSF kiasi cha zaidi ya Bilioni 3.
Akizungumza mbele ya Waandishi wa Habari mapema leo Februari 3. 2022, Katibu wa waliokuwa wafanyakazi wa New Habari (2006) Ltd, Arodia Peter alisema licha ya kusubiria kwa muda mrefu taratibu za kisheria dhidi ya mfanyabiashara huyo pamoja na Mbunge wa Nzega Mjini ambaye pia ni Waziri wa Kilimo Hussein Bashe kushindwa kuwasilisha mafao yao kwenye mifuko licha ya kuwakata michango kwa miaka zaidi ya 10.
"Walikuwa wanatukata mishahara yetu kila mwezi pamoja na michango ya mwajiri kwa mujibu wa sheria kwa zaidi ya miaka 10.
Licha ya kuhoji, Mwajili alituhaminisha kuwa anapeleka makato yetu katika mifuko husika...
Lakini tunashangaa Watendaji wa mifuko hiyo kutochukua hatua yoyote kwa mwajiri kwa zaidi ya miaka 10 tofauti na sheria ya mifuko hiyo unayoelekeza." Alisema Arodia.
Na kuongeza kuwa;
"Tunapenda kufikisha taarifa na kilio chetu kwa Rais Samia Suluhu Hassan juu ya madhila yanayotupata na yanayoendelea dhidi ya Rostam Aziz na Afisa Mtendaji Mkuu, Mbunge na Waziri wa kilimo Hussein Bashe kwani wameshindwa kabisa kutupelekea mafao yetu katika mifuko ya Hifadhi ya Jamii." alisema Arodia.
Rostam Aziz na Hussein Bashe walituondoa kazini Mei 31 mwaka 2019 bila kutulipa stahiki za mafao yetu kwa mifuko ya NSSF na PSSSF kwa mujibu wa Sheria.
Ambapo alifafanua kuwa; Mtendaji mkuu Hussein Bashe, aliwaondoa kazini kwa lazima wafanyakazi wote bila kutangaza kwa umma sababu ya kufanya hivyo kama sheria inavyotaka.
Kwa upande wake Mshauri katika kikao hicho waliokuwa wafanyakazi wa New Habari (2006), Mzee Balinagwe Mwambungu alitoa kilio chake kwa wadaiwa hao Rostam Aziz na Hussein Bashe, kuwa kwa sasa wanaishi kwa mateso huku pesa zao zikiwa zipo kwa wadaiwa.
"Wapo wenzetu wametangulia mbele za haki na familia zao tuonao hapa wakidai malipo ya wapendwa wao.
Waliotangulia mbele za haki ni pamoja na: Aliyekiwa Mhariri Kanda ya Kaskazini, Elia Mbonea, Mhariri wa Maudhui ya Habari wa kampumi, Mwalimu Chrysotom Rweyemamu, Mhariri wa Habari wa gazeti la Rai, Innocent Mnyuku, Mhariri wa Makala wa gazeti la Rai, Mayege Mayege, Mhariri wa michezo, Asha Muhaji.
Pia wengine Afisa Utawala Msaidizi, Benjamin Mhina pamoja na Katibu Muhtasi Roida Kiverege. Hawa wote wametangulia mbele za haki na bado wanadai mafao yao kupitia kwa familia zao ambazo zinaishi kwa shida" alisema Mzee Mwambungu.
Hata hivyo kwa kauli moja wawakilishi hao wametangaza kufanya maandamano ya amani yasiyokuwa na ukomo nyumbani kwa Rostam Aziz na ofisini kwake, na pia maandamano hayo ya amani kwa Hussein Bashe na ofisini kwenye mifuko ya hifadhi ya Jamii.
Wafanyakazi hao zaidi ya 200 ni pamoja kutoka Tanzania nzima wakiweno Waandishi wa habari ambao ndo kundi kubwa, watu wa IT, Madereva, Walinzi, wafagiaji, mafundi mitambo na wengine wengi.
0 Comments