Na Fatma Ally MDTV Dar es Salaam
Makamo wa Kwanza wa Rais ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, ambae pia ni Makamo Mwenyekiti wa ACT Wazalendo, Othman Maoud Othman, amesema, kuwa kwake kimya hakumanishi kuwa amenyimwa nafasi na cheo alichonacho au hakuna kinachofanyika bali atakapotimiza mwaka mmoja wa uongozi wake atazungumzia mafanikio na changamoto waliyoyapata ndani ya Serikali.
Kauli hiyo ameitoa jijini Dar es Salaam wakati alipokua akizungumza na waandishi wa habari ikiwa ni siku chache tangu kuteuliwa na chama chake kuwa Makamo Mwenyekiti Zanzibar.
Amesema kuwa, katika uongozi wake atahakikisha anawaunganisha wanachama wote kuwa pamoja na kushirikiana katika shughuli za kijamii na kisiasa na kukataa kuwepo makundi ndani ya chama.
Hata hivyo, amesema atahakikisha anasimamia mariadhiano ya kisiasa yalioasisiwa na mtangulizi wake Hayyat Maalim Seif Shariff Hamadi, hivyo chama hicho kitabaki kupigania haki za kijamii, kisiasa na ustawi wa kiuchumi kwa wananchi wote, ambayo hayo yatafikiwa endapo watasimamia kwa dhati mariadhiano ya kisiasa.
Sambamba na hayo pia atasimamia uwajibikaji wa kitaasisi ambapo kila kiongozi wa Chama wa ngazi yoyote kuanzia tawi hadi Taifa, pamoja na kuhuisha utamaduni wa kukifanya chama chao kuwa chemuchemu ya fikra mbadaka kwa kuibua hoja na kuanzisha mijadala ya kitaifa.
Ameongeza kuwa, miongoni mwa mambo yanayohitajika baada ya kujiunga na Serikali ya Umoja wa kitaifa ni pamoja na kufanyia mabadiliko mfumo wa uchaguzi Ili kuwa na mfumo wa uchaguzi utakaohakikisha uchaguzi huru.
Hata hivyo, amesema watahakikisha wanarejesha Imani ya wananchi na Serikali na mfumo mzima wa Uendeshaji wa nchi kwa kufanya uchaguzi huru pamoja na kujenga Serikali yenye ufanisi na kuimarisha misingi ya utawala bora na uwajibikaji katika Uendeshaji wa Serikali.
Hata hivyo, amesema kupitia uzoefu wake atashirikiana na viongozi wenzake kujipanga kimkakati kuhakikisha kuwa ACT inashiriki vyema uchaguzi Mkuu 2025 na kuvuka vikwazo vyote vilivyowazuia miaka ya nyuma kuunda Serikali.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama Cha ACT Wazalendo Juma Duni Haji amesema hawezi kuziba nafasi ya aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama hicho Hayyat Maalim Seif Shariff Hamadi.
Amesema kuwa, Hayyat Maalim Seif hakua kiongozi wa kawaida, huku akieleza kwamba viongozi wa aina yake hutokea mara chache duniani, hivyo ameeomba asilinganishwe naye kwani hawafanani .
"Lakini nawahakikishia kuwa nami nina uzoefu wa muda mrefu wa kutosha na wa maarifa ya kutosha ambayo nitayatumia katika kukiongoza chama Cha ACT katika kufikia mafanikio ya kushika dola na kuwakomboa watanzania kiuchumi, kisiasa na kijamii"amesema Duni.
Aidha, amesema kuwa kuna mambo ambayo atayapa kipaumbele katika uongozi wake ikiwemo kusimamia mageuzi ya Uendeshaji wa Chama kisasa, Kudai tume huru ya uchaguzi na katiba mpya,kuendeleza siasa za masuala, ujenzi wa Taasisi,kupigania na kutetea haki, umoja na mariadhiano.
Hata hivyo, amesema kulingana na nafasi ya uongozi aliyonayo itakua rahisi kuweza kumfikia Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kuweza kumueleza mambo mbalimbali yanayowahusu wananchi.





0 Comments