Header Ads Widget

MADIWANI HALMASHAURI YA MULEBA WATAKIWA KUHAMASISHA WANANCHI ANWANI ZA MAKAZI


MADIWANI wa halmashauri ya wilaya ya Muleba mkoani Kagera wameaswa kuhamasisha wananchi katika kata zao, kushiriki kikamilifu katika zoezi la uwekaji wa anwani za makazi, ili kurahisisha kazi hiyo na kuiwezesha kufanyika kwa ufanisi.


Akizungumza katika kikao cha baraza la madiwani wa halmshauri ya wilaya hiyo cha kujadili taarifa za robo ya pili ya mwaka inayoanzia Oktoba hadi Desemba 2021, Mkuu wa Wilaya ya Muleba, Toba Nguvulla alisema kuwa endapo madiwani hao watatumia nyadhifa zao kuwahamasisha wananchi, zoezi hilo litafanyika kwa haraka na kukamilika katika muda ulipangwa.


"Kama mlivyofanya kazi kubwa ya kuhamasisha wananchi wajitokeze kupata chanjo ya ugonjwa wa Uviko 19 na kufanikisha hilo kwa kiwango kikubwa, nawaomba pia mfanye hivyo ili kuhamasisha wananchi waliowachagua washikiri kikamilifu katika zoezi la uwekaji anwani za makazi, bila kujali tofauti zenu za kiitikadi maana maendeleo hayana chama" alisema. 


Akiwasilisha kwa niaba ya mkurugenzi taarifa ya mafunzo ya kujengewa uwezo kwa watalaamu wa halmashauri ya wilaya hiyo kuhusu mfumo huo wa anwani za makazi, mhandisi wa ujenzi Charles Solo aliiasa jamii kupokea mfumo huo maana ni muhimu katika maendeleo endelevu ya mtu mmoja mmoja na jamii nzima kwa ujumla.

"Zipo fursa nyingi zitakuwepo endapo mfumo huu utafanikiwa kama ilivyokusudiwa, maana wananchi wanaweza kuutumia hata kufanya biashara za mtandaoni kutokana na upatikanaji wao kuwa rahisi, lakini pia ni muhimu katika masuala ya usalama mfano ikitokea ajali ya moto, ni rahisi kuwaelekeza zimamoto wakafika kwa wakati na kunusuru mali na maisha ya watu" alisema.

Mhandisi Solo alisema kuwa dhamira ya serikali ni kukamilisha utekelezaji wa awani hizo za makazi kabla ama ifikapo mwezi Mei 2022, kwa kuhakikisha kila nyumba ama jengo linakuwa na anwani ya makazi, na kwamba endapo wananchi na wadau wengine watatoa ushirikiano wa kutosha, kazi hiyo itakamilika kwa wakati.




Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI