NA AMON MTEGA, SONGEA.
CHUO cha Taifa cha Utalii kimetoa mafunzo ya siku tano ya UVIKO 19 kwa wadau zaidi ya 140 wa huduma za utalii wa Mkoani Ruvuma ili kuwajengea uwezo wa kuwahudumia wageni (Watalii) pindi wanapoenda kutembelea kwenye vivutio mbalimbali vya mkoani humo.
Akizungumza Mkuu wa Chuo cha Taifa cha Utalii Dkt,Shogo Sedoyeka wakati wa uzinduzi wa mafunzo hayo amesema kuwa yamefadhiliwa na mpango wa maendeleo kwa ustawi wa Taifa na makabiliano dhidi ya UVIKO 19 kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii.
Dkt ,Sedoyeka amesema kuwa Chuo kimeamua kutoa mafunzo hayo kwa wadau wa utoaji wa huduma za Utalii baada ya kubaini kuwa baadhi yao walikuwa bado hawana uelewa wa kutosha kuhusiana na Uviko 19 pindi wanapowahudumia watalii .
Amesema kuwa mafunzo hayo yatatolewa kwenye mikoa nane na hadi sasa mikoa minne ambayo ni Ruvuma ,Mtwara ,Lindi na Njombe imeshafanyiwa mafunzo hayo huku mikoa minne iliyobaki na yenyewe itafikiwa.
Aidha katika hatua nyingine Dkt Sedoyeka amempongeza Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha hizo ambazo zinawezesha kukabiliana na Uviko 19 kwenye jamii pamoja kuwajali watalii ili wageni wapatiwe huduma bora .
Kwa upande wake Katibu Tawala wa Mkoa wa Ruvuma Steven Ndaki ambaye alimwakilisha mkuu wa mkoa huo Brigedia Wilbert Ibuge kwenye uzinduzi huo katika nafasi ya mgeni rasmi amesema kuwa sekta ya utalii imekuwa ikitoa fursa mbalimbali ikiwemo suala la ajira hivyo inatakiwa kuizingatia kikamilifu .
Ndaki amesema kuwa katika kipindi cha janga kubwa la Corona utalii uliyumba katika Nchi mbalimbali hivyo kwa sasa inatakiwa kuitumia elimu ya Uviko 19 ipasavyo ili kulinda watalii na jamii kwa ujumla .
Naye Maajabu Mbogo Afisa Utalii katika pori la Limbaramba alisema kuwa mafunzo hayo yataleta neema ya kuongezeka kwa watalii na kuifanya Serikali iweze kupata mapato kupitia watalii hao.
Hatahivyo Mbogo ameishukuru Serikali kwa kutambua umuhimu wa mafunzo hayo kwa wadau wa utalii kwani kufanya hivyo kutajenga mshikamano wa pamoja baina ya wadau hao pamoja nawafanyakazi wa sekta ya utalii namna ya kuwahudumia wageni.
Mmoja waliopatiwa mafunzo hayo Bernad Lisambo kutoka Wilaya ya Nyasa amesema kuwa mafunzo hayo yatawapa uzoefu wa kutoa huduma kwa wageni ambao ni watalii.
0 Comments