Header Ads Widget

WATAALAM NA WATENDAJI KATIKA HALMASHAURI ZA MKOA WA KIGOMA WAMETAKIWA KUSIMAMIA MIRADI KWA WELEDI NA KUTOA TAARIFA SAHIHI

 .


 


MJUMBE wa halmashauri kuu ya CCM Taifa kutoka mkoa Kigoma Abdulkadri Mushi amewataka watendaji na wataalam katika halmashauri za mkoa Kigoma kusimamia miradi kwa weredi na kutoa taarifa za hali halisi za miradi wageni wanapotembelea miradi hiyo badala ya kuficha taarifa za changamoto zinazoikabili miradi.


Mushi alisema hayo wilayani Buhigwe mkoani Kigoma akiongoza wajumbe wa kamati ya siasa ya mkoa huo kutembelea na kukagua miradi mbalimbali ya wananchi ikiwa ni kukagua utekelezaji wa ilani ya Uchaguzi ya CCM na kusema kuwa taarifa sahihi ndiyo jambo pekee linaloweza kufanya miradi yenye changamoto kupata suluhu ya namna ya kuitekeleza ili iweze kukamilika.


Mjumbe huyo wa halmashauri kuu ya Taifa ya CCM alieleza kutoridhwa na taarifa za utekelezaji wa miradi ya maji Mwayaya, zahanati ya kijiji cha Bweranka, barabara ya lami mita 800 ahadi ya Raisi wakati wa uchaguzi  na ujenzi wa mradi wa maji katika kijiji cha Migongo -  Kilelema.


Akiwa katika kijiji cha Bweranka na Migongo Mjumbe huyo wa NEC aliwaeleza viongozi hao kwamba wameshindwa kusimamia majukumu yao hasa kushindwa kuwa na taarifa za mpango wa ujenzi wa mradi (BoQ) huku wakishindwa kujua tahamni ya utekelezaji wa miradi hiyo na kiasi kinachohitajika ili kuifanya miradi hiyo ya muda mrefu kukamilika.


Ili kuwezesha kupata taarifa za miradi hiyo ameelekeza kuundwa kwa kamati ndogo ya wataalam kufuatilia kwa undani na kuwa na taarifa za kina za gharama halisi zilizotumika hadi sasa na kiasi kinachohitajika kumalizia miradi hiyo huku akitoa siku 14 kupata taarifa hiyo.


Hata hivyo Mushi alieleza kuvutiwa na jitihada za wananchi wa kijiji cha Bweranka kwa jitihada zao za kujitoa kuanza utekelezaji wa zahanati kijijini hapo bila msaada kutoka popote hadi Raisi Samia alipoa shilingi milioni 50 kuunga mkono ujenzi huo ambapo Mjumbe huyo wa NEC alitoa shilingi milioni tatu kuunga mkono jitihada hizo.



Akizungumzia hali hiyo Mhandisi wa ujenzi wa halmashauri ya wilaya Buhigwe, Jerry Mwakapemba alisema kuwa baadhi ya miradi hiyo ilikuwa nje ya utaratibu wa usimamizi wa halmashauri hiyo ikirithiwa kutoka iliyokuwa wilaya ya Kasulu hivyo kufanya kutokuwepo kwa taarifa za kuanza kwa miradi hiyo na gharama zake.


Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri ya wilaya Buhigwe, Essau Hosiana akizungumza wakati wa majumuisho ya ziara hiyo alisema kuwa amechukua maelekezo ya Mjumbe huyo wa NEC na kwamba watayafanyia kazi na kutoa taarifa kwa mamlaka zinazohusika.


Hosiana amekiri kuwepo kwa changamoto za utekelezaji wa miradi hiyo na kwamba wataunda kikosi cha wataalam ambacho kitapitia miradi hiyo na kuwa na taarifa za kina za kuanzishwa kwake, changamoto na mapendekezo ya nini kifanyike kuwezesha miradi hiyo kukamilika.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI