Header Ads Widget

UONGOZI SHULE ZA MKOA WA PWANI WATAKIWA KULINDA MADARASA YALIYOJENGWA KWA FEDHA ZA UVIKO_19







CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) mkoa wa Pwani kimeutaka uongozi wa shule za mkoa huo kuyalinda madarasa yaliyojengwa fedha zitokanazo na mapambano ya ugonjwa wa Covid-19 yalindwe na wasiyatmie vibaya ili kuepuka uharibifu.


Akizungumza baada ya kufanya ziara kwenye shule ambazo zimepata mradi wa fedha hizo kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya madarasa kwa shule za sekondari na shule shikizi za msingi kwenye baadhi ya shule kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha mwenyekiti wa CCM mkoa wa Pwani Ramadhan Maneno alisema kuwa fedha zilizotolewa ni nyingi na zinapaswa kulindwa.


Maneno alisema kuwa chama kimeridhishwa na ujenzi wa madarasa hayo na yatasaidia kukabiliana na upungufu wa vyumba vya madarasa ambapo wanafunzi walikuwa wakisongamana na baadhi walikuwa wakikosa nafasi ya kujiunga na kidato cha kwanza.


"Naipongeza awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan ambapo imehakikisha inapata fedha kwa ajili ya kuhakikisha watoto wanasoma kwenye mazingira mazuri na kuitekeleza ilani ya chama hivyo uongozi unapaswa kuhakikisha unatunza madarasa haya,"alisema Maneno.


Kwa upande wake kaimu mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha Shukuru Lusanjala alisema kuwa baada ya zoezi la ujenzi wa vyumba vya madarasa 20 kwa shule za sekondari na vyumba 10 kwa shule shikizi yenye thamani ya shilingi milioni 600 kukamilika tayari wameanza kutengeneza madawati 791 ambapo Halmashauri imetoa milioni 79 utengenezaji wa madawati kwa ajili ya shule zote.


Naye ofisa elimu sekondari Fatuma Kisalazo alisema kuwa hawana changamoto ya walimu kwenye shule ukiachilia uhaba wa walimu wa masomo ya Sayansi.


Naye Mwalimu mkuu msaidizi wa Shule ya Sekondari Kilangalanga Salum Malegi alisema kuwa wanaipongeza serikali kwa kutoa fedha hizo kwa ajili ya kujenga madarasa hayo kwani itasaidia kupunguza changamoto ya upungufu wa madarasa.


Mwenyekiti huyo katika ziara yake ambapo aliambatana na uongozi wa CCM Wilaya ya Kibaha Vijijini na uongozi wa Halmashauri walitembelea Shule za Sekondari Kilangalanga, Kawawa na Disunyala na Shule Shikizi ya Mkombozi.



Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI