Imeelezwa kuwa miongoni mwa sababu zinazopelekea kutokea mafuriko ya mara kwa mara mvua zinaponyesha jijini Dar es Salaam ni ujengaji holela wa nyumba na utupaji wa taka ovyo kwenye mifereji hali inayopelekea kuziba kwa njia za maji. ......Na Fatma Ally, MDTV Dar es salaam
Hayo yamebainishwa na Meneja wa Tarura mkoa wa Dar es Salaam Eng Geofrey Mkinga wakati akizungumza na Mtandao wa Matukio Daima ulipotaka kufahamu sababu zinazopelekea kuwepo kwa mafuriko Dar es Salaam licha ya kufanyika maboresho kwenye Miundombinu.
Amesema kuwa, changamoto kubwa inayosababisha mafuriko katika Jiji hilo, ni watu kuvamia sehemu za njia za maji hali inayopelekea maji kukosa njia ya kupitia na kusambaa kwenye maeneo ya makazi ya watu.
"Utaskia watu wanasema kwamba zamani maji hayo hayakuepo lakini tangu kujengwa kwa mifereji kumekua na mafuriko sehemu nyingi,hii yote inasababishwa na watu kujenga kiholela kwenye njia za maji na kutupa taka ovyo, kwani taka zinapojaa zinaziba njia za maji"amesema Eng Mkinga.
Aidha amesema kuwa suala la Miundombinu hasa ya barabara ni suala mtambuka ambalo linajumuisha ofisi mbalimbali ikiwemo watu wa Mipango miji, Tanroad, Tarura pamoja na Baraza la Mazingira (Nemc), hivyo Ili kutatua changamoto hiyo wamekua wakikutana Ili kujadili kwa pamoja namna watakavyomaliza changamoto hiyo.
Hata hivyo, amesema ni vyema watu kujenga mita 60 mpaka 30 kuanzia vilipo vyanzo vya maji Ili kuepusha changamoto za mafuriko hasa yanayotokana na uvamizi wa njia za maji kama inavyooneka katika maeneo mengi jijini Dar es Salaam.





0 Comments