Baadhi ya jamii zimekuwa zikichukulia kuwa wanawake kufanya kazi za kuchezesha muziki(DJ) ni uhuni kwani kazi hiyo ilizoeleka kufanyanywa na wanaume peke yao jambo ambalo sio kweli kwani hata wanawake wanaweza kuifanya kazi hiyo na kujiingiza kipato......NA NAMNYAK KIVUYO, ARUSHA
Hayo yalisemwa na Dj Magdalena Adolf Inju(Dj Maggie) anayefanya kazi zake za kuchezesha muziki Katika mikoa mbalimbali ikiwemo Arusha, Dar es salaam na Mwanza ambapo alisema kuwa pamoja na kwamba kazi hiyo ni rahisi kuzifanya imekuwa na changamoto kwa wanawake kutokana na mtazamo hasi uliopo katika jamii kuwa kazi hiyo inafanywa na wanaume tu na endapo mwanamke ataifanya basi atakuwa muhuni.
“Mwanamke kufanya kazi hii sio uhuni na mimi kwa kuzifanya nimeionyesha jamii kupitia kipaji changu kuwa udj sio umalaya au uhuni bali ni kazi kama zilivyo kazi nyingine na inanifanya napata pesa kwaajili ya kuendesha maisha yangu siibi wala sinyang'anyi kupitia kazi hii nakula na naishi vizuri,” Alisema Dj Maggie.
“Kuna watu katika jamii wanasema kuwa kutokana na kazi za udj anazofanya mwanamke hawezi kuwa mwanamke bora kwani atashindwa kufanya mambo mengine ikiwemo kuwa mke na shughuli za nyumbani ambazo kwa tamaduni za Afrika zimekuwa zikifanywa na wanawake pekee kama vile kupika, kufanya usafi na kutunza familia lakini sio kweli kwani mimi pamoja na kufanya kazi ya hii na kama ilivyozoeleka inafanyika usiku naweza kutekeleza na majukumu yangu yote ya nyumbani bila shida yoyote kikubwa ni kupangilia muda tuu,” Alifafanua.
Alieleza kuwa pamoja na kazi hiyo kuwa rahisi kufanywa na mtu wa jinsia yoyote kama mwanamke anakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo kutoaminiwa katika utendaji wa kazi kwasababu tu niwanamke , kuombwa Rushwa ya ngono na baadhi ya watu wanaowaomba kazi, watu kugombana eneo na kuanza kurusha chupa jambo linalohatarisha usalama pamoja na kudharauliwa kwasababu tu ni mwanamke na wakati mwingine hata wanawake wenzao wanawadharau na kuona hawawezi kufanya chochote.
“Unakuta unapanda stejini kwaajili ya kusherehesha unasikia wenzio wanasema sasa huyu atafanya nini hapo lakini baada wakukubali kwahiyo kikubwa niwaambie akina dada wasiogope kuzifanya kazi hii kwani cha kwanza kabisa ni kazi rahisi na pili inaweza kukuingizia kipato na ukaendesha maisha yako na kuwa na maendeleo kama kazi nyingine tuu,”Alieleza Dj Maggie.
Alisema kuwa mwanzoni wakati anaanza kufanya kazi hiyo ilikuwa ngumu hasa kuwaambia wazazi kuwa nafanya kazi za kuchezesha muziki wakati katika jamii kazi hiyo inaonekana kuwa ni kazi isiyo na heshima kwa wanawake lakini kutokana na jitihada zake za na uthubutu aliokuwa nao waliona ameanza kubadilika kimaisha kWa kuwa na maendeleo fulani lakini pia kuona kuwa pamoja na kufanya kazi hiyo hajabadilika tabia na kuwa muhuni walimuunga mkono na mpaka Sasa anafanya kazi huku familia yake ikiwa nyuma yake kumsaidia atimize malengo aliyonayo.
“Mwanzo ilikuwa ngumu kuwaelewesha wazai wangu lakini sasa hivi wanapost hadi matangazo yangu ya kazi na wadada niwaambie tuu kama una kipaji cha kufanya kazi hii fanya Wala usiogope changamoto hakuna kazi isiyo na changamoto mimi niliamua na mpaka Sasa nimefanya kazi ambazo ni kubwa kazi ambayo siaamini kama niliomba na nikapata na kufanya katika viwango vya hali ya juu,” aliendelea kusema.
Kwa upande wa baadhi ya wanajamii Winifrida Tety mkazi wa Arusha alisema kuwa ni kweli ni ngumu kumuamini mwanamke kuwa anaweza kufanya kazi hiyo na hasa ni kwasababu zinafanyika usiku mimi pia najiuliza atafanya kazi za nyumbani muda gani ataangalieje familia maana usiku yupo kazini kwa maana hiyo asubuhi na mchana atapaswa kulala lakini tunaona wengi wanafanya na sio kwenye nyumba za burudani duu lakini pia kwenye radio na television ambazo hizi haziwabani kufanya usiku lakini pia pale wanapohitajika kufanya usiku nafiki wanajiandaa na kuweka mambo sawa.
“Watu ni ngumu kuelewa lakini Mimi pia nawaunga ma Dj wanawake mkono kwasababu kama wanapata pesa kwanini wasifanye kikubwa ni mkono uende kinywani na maisha yaendelee na ni bora kufanya kazi hii kuliko kubaki tu nyumbani kuomba omba kwenda kujiuza mi nafikiri jamii kwa Sasa ibadili mitazamo inayowwgandamiza wanawake na kuwafanya washindwe kuzifikia ndoto zao,” Alisema.
Naye Alfred Zakaria mkazi wa kata ya Musa Arusha alisema kuwa kazi hiyo wamekuwa wakiisikia lakini kuona ikifanya katika sherehe mbalimbali kama harusi, ubarikio na matukio mengine mengi ikiwemo misiba na wameona kuwa ni huduma ambayo jamii inahitaji kwa asilimia kubwa hivyo yeye anaona ni sawa ikifanya na jinsi zote ilimradi malengo ya kazi yafikiwe.





0 Comments