Header Ads Widget

MTOTO MMOJA AFARIKI WENGINE WAJERUHIWA KWA KUFUKIWA NA KIFUSI WAKATI WAKICHIMBA MCHANGA KUPATA FEDHA ZA MAHITAJI YA SHULE

Mtoto Justine Abson (14) amefariki dunia, wakati yeye na mwenzake wakichimba mchanga kwa ajili ya kuuza ili wapate fedha za kununulia mahitaji ya shule, ikiwamo madaftali na viatu.


 Akizungumzia tukio hilo mkuu wa wilaya ya Muleba mkoani Kagera, Toba Nguvila amesema kuwa tukio hilo lilitokea Ijumaa wiki hii saa 3:30 asubuhi, katika kijiji cha Buhaya kata Kagoma wilayani humo.


Nguvila amesema kuwa mtoto Carlos Shubi (14) amejeruhiwa sehemu mbalimbali za mwili wake ikiwamo miguuni na mgongoni, na kwamba amelazwa katika hospitali ya Kagondo na anaendelea kupatiwa matibabu.


Amesema kuwa watoto hao walikuwa wamechaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza katika shule ya sekondari Buhaya, ambayo ni shule mpya iliyojengwa kwa fedha za Uviko 19, na kwamba walikuwa wanatafuta pesa kwa ajili ya kununulia mahitaji ya shule ili Jumatatu (Januari 25, 2022) waende kuanza masomo.


"Taarifa za watoto hao kufukiwa na kifusi cha mchanga zilitolewa na wananchi, tulijitahidi kuokoa maisha yao lakini  walipotolewa kwenye kifusi hicho tayari mtoto Justine alikuwa amekwishapoteza maisha" amesema Nguvila


Amesema mtoto Carlos amejeruhiwa sehemu za miguuni na mgongoni na bahati nzuri ameonekana kutovunjika mifupa, lakini kuna sehemu za mwili wake nyama zimetoka, huku akimwombea kupona haraka ili  ajiunge na wenzake ambao tayari wameanza masomo katika shule ya sekondari Buhaya.


"Chanzo cha ajali hii ni ardhi ya eneo hilo kuwa na maji mengi kufuatia mvua zinazonyesha, hali iliyosababisha kuwepo kwa mipasuko mingi na kusababisha kukatika kwa gema na kuwafukia watoto hawa wakiwa wanachimba mchanga" amesema.


Kufuatia tukio hilo mkuu huyo wa wilaya amelifunga eneo hilo na kupiga marufuku mwananchi yeyote asiende kuchimba mchanga katika eneo hilo hatarishi.









Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI