Miradi mbalimbali ya kimaendeleo katika jimbo la Moshi Vijijijini mkoani Kilimanjaro inatarajiwa kuanza kwa utekelezaji wake mara moja baada ya serikali kuu kutoa fedha kiasi cha shilingi Milioni 49 .7 kwa ajili ya kuitekeleza Mwandishi wa Matukio Daima Gift Mongi anaripoti kutoka Moshi
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Moshi mbunge wa jimbo hilo Profesa Patrick Ndakidemi amesema kupatikana kwa kiasi hicho cha fedha kutaenda kumalizia miradi mbalimbali katika kata ikiwemo ile iliyoanzishwa kwa nguvu za wananchi.
Kwa mujibu wa Prof Ndakidemi ni kuwa serikali kuu ilipokea maombi kutoka katika kata zote 16 zilizopo ndani ya jimbo hilo na walipokea miradi 30 ambayo inapaswa kukamika ndani ya kata hizo.
Alisema kutokana na mgawanyo ulivyo kila kata itaenda kupata kiasi cha milioni 3 na kuwa miongoni mwa miradi iliyopewa kipaumbele ni ile ya vyoo katika shule za msingi na zahanati, na kusema kila Kata imepata Milioni 3 ,huku Kata ya Kibosho Kati ikipata zaidi ya Shilingi Milioni 4.
"Fedha hizi zitaenda kwa mgawanyo ulio sawa kwa kwa mantiki hiyo ni kama kila kata itaenda kupata wastani wa milioni 3 hivi lakini tunaenda kutekeleza ile miradi ambayo imeshaanza tayari ili tumalizie viporo kabla ya kuanzisha mwingine" alisema
Katika hatua nyingine Prof Ndakidemi aliwataka wananchi kuacha dhana ya kuisubiri serikali kuwaletea maendeleo na badala yake waongeze nguvu katika kuchangia shughuli za maendeleo ili waweze kukamilisha miradi hiyo iliyopo ndani ya kata hizo kwa wakati.
"Ikumbukwe kuwa serikali ina mambo Mengi hivyo tusikae kwa kubweteka kusubiri itufanyie kila kitu badala take tuone umuhimu katika kujitolea na kuchangia shughuli za maendeleo na pale tutakapokwama ndipo serikali ije itushike mkono sasa" alisema Mbunge huyo.
Mwisho.
0 Comments