Header Ads Widget

MADIWANI HALMASHAURI YA MOSHI WAKERWA NA UWEKAJI WA MATUTA BARABARANI KIHOLELA



Na WILLIUM PAUL, Moshi.


BARAZA la Madiwani halmashauri ya Moshi mkoani Kilimanjaro limeonyesha kukerwa na vitendo vya wananchi kuweka matuta barabarani hovyo hali inayopelekea kuharibu magari na wakati mwingine kupelekea kutokea kwa ajali.

 


Wamedai kuwa lipo tatizo jingine la wananchi kupitisha mifugo katika barabara zilizojengwa na kupelekea barabara hizo kuharibika mapema.

 

Hayo yameibuka katika kikao cha Baraza maalum la kujadili utekelezaji wa bajeti ya Wakala wa barabara vijijini na mijini (TARURA) pamoja na wakala wa maji (RUWASA) kwa mwaka wa fedha 2021/2022 na bajeti yam waka mpya wa fedha 2022/2023.

 


Mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Moris Makoi alisema kuwa, wananchi wamekuwa wakijichukulia sheria mkononi kwa kuweka matuta barabarani huku mengine hayana viwango wala alama maalum inayoonyesha uwepo wa tuta hilo.

 

Alisema kuwa, hali hii imekuwa ikisababisha adha kubwa kwa wamiliki wa magari kwani matuta hayo yamekuwa yakipelekea magari kuharibika na wakati mwingine kupelekea ajali zisizotegemewa.

 


“Yapo matuta mengine yanayowekwa na wananchi ni makubwa na hakuna alama yoyote inayoashiria uwepo wa tuta hivyo inapelekea magari kuharibika kwa kupanda katika matuta hayo na wakati mwingine kupelekea ajali zisizo za lazima” alisema Makoi.

 

Mwenyekiti huyo aliwataka TARURA kuhakikisha wanasimamia sheria zilizowekwa kwa ajili ya kuzilinda barabara hizo ikiwamo kuwachukulia hatua wananchi wanaoweka matuta bila kuwa na kibali kutoka Tarura pamoja na wale wanaopitisha mifugo katika barabara.

 


Akijibu hoja hizo, Meneja wa Tarura wilaya ya Moshi, Mhandisi Africano Orota alisema kuwa, kwa mujibu wa sheria wananchi hawaruhusiwi kufanya chochot katika maeneo ya barabara ikiwamo uwekaji wa matatu na wenye jukumu la kufanya hivyo ni Tarura.

 


“Kwa mujibu wa sheria za barabara wananchi hawaruhusiwi kufanya chochote katika eneo la barabara na kama kunauhitaji wa tuta wanapaswa kuja Tarura kuomba ambapo tutatuma wataalam wetu kwenda kuona kama eneo husika linauhitaji wa tuta na wenyekuweka tuta hilo ni sisi na sio wananchi” alisema Mhandisi Orota.

 


Aliongeza kuwa, kwa mujibu wa sheria za barabarani Mwananchi atakayekiuka sheria na kuweka tuta atatozwa faini ya shilingi laki tano au kifungo cha mwaka mmoja jela au vyote kwa pamoja.


Aidha kwa mifugo itakayokuwa ikipitishwa katika barabara itatozwa faini ya shilingi laki tano kwa kila mfungo na kutumia nafasi hiyo kuwaomba Madiwani na viongozi wa vijiji na kata kuwaelimisha wananchi ili kuepuka adhabu hiyo.



Katika baraza hilo Madiwani hao walipitisha bajeti ya mwaka wa fedha 2022/2023 kwa Tarura Bilioni 4.3 huku kwa upande wa Ruwasa wakipitisha bajeti ya Bilioni 3.9.


Mwisho...

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI