Na WILLIUM PAUL, MOSHI.
MKUU wa wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro, Abbas Kayanda amewataka mafundi waliopewa kazi ya ujenzi wa shule ya sekondari ya Njia panda kuhakikisha wanakamilisha kazi hiyo kwa wakati huku wakizigatia thamani ya fedha.
Kayanda ametoa kauli hiyo jana wakati wa uzinduzi wa ujenzi wa shule hiyo ambapo alisema kuwa, serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hasani imeshatoa fedha milioni 470 kwa ajili ya ujenzi wa shule hiyo ya sekondari.
Alisema kuwa, ujenzi wa shule hiyo umeanza rasmi ambapo mafundi wamepewa miezi mitatu kuhakikisha majengo hayo yanakamilika na kuyakabidhi ifikapo Aprili 30 mwaka huu.
“Katika ujenzi wa shule hii tutajenga madarasa nane, maabara tatu na jengo la utawala moja na jengo la kompyuta ambapo waanchi wamejitolea kuchimba msingi baada ya kuhamasiswa kutoa nguvu kazi yao ili kuhakikisha ujenzi unakamilika kwa wakati” alisema Kayanda.
Mkuu huyo wa wilaya aliwataka mafundi kukamilisha ujenzi huo kwa wakati kama walivyokubaliana katika mikataba yao na kuzingatia thamani ya fedha katika kila jengo huku akimuagiza Mhandisi wa wilaya kuhakikisha anasimamia ujenzi huo.
Alisema kuwa, kukamilika kwa majengo hayo yatasaidia wakazi wa kata ya Njia panda ambapo watoto wao wamekuwa wakitembea umbali mrefu kufuata shule ya sekondari.
Aidha Mkuu huyo wa wilaya aliwaomba Wananchi kuwa walinzi namba moja ya vifaa vitakavyokuwa vikiletwa kwa ajili ya ujenzi wa shule hiyo pamoja na kuwapa ushirikiano mafundi ili kuhakikisha kuwa ujenz huo unakamilika kwa wakati.
Kwa upande wake, Mtendaji wa kata ya Njia panda, Elisha Mushi alisema kuwa, wananchi wameonyesha mwitikio mkubwa wa ujenzi wa shule hiyo kwa kujitoa nguvu kazi kwani kulikuwa na uhitaji mkubwa wa shule ya sekondari.
Mushi alisema kuwa, mradi huo wa ujenzi wa shule ya sekondari utagharimu milioni 600 ambapo kwa sasa serikali imetoa milioni 470 na kuda kuwa uhitaji wa shule hiyo ni mkubwa kwani wanafunzi wamekuwa wakitembea umbali wa kilomita 5 mpaka kilomita 7 kufuata huduma ya shule katika kata ya Makuyuni na Kahe.
“Kutokana na wanafunzi kutembea umbali mrefu kufuata sekondari imepelekea wanafunzi wengi kukatiza masomo yao kutokana na kurubuniwa na kubeba mimba huku wanafunzi wa kiume wakijiingiza katika makundi maovu ya uvutaji bangi pamoja na ulevi hivyo ujio wa shule hii utasaidia kuondoa tatizo hili” alisema Mushi.
Naye Diwani wa kata ya Njia panda, Loveness Mfinanga alitumia nafasi hiyo kumshukuru Rais Samia Suluhu Hasani kwa kuleta fedha kwa ajili ya ujenzi wa shule hiyo.
Loveness alisema kuwa, watoto wa kata hiyo wamekuwa wakikumbana na changamoto kubwa ya kutembea umbali mrefu kufuata shule ya sekondari hali ambayo imekuwa ikipelekea wananchi kufanya vibaya.
Alisema kuwa, ujenzi wa shule hiyo utasaidia kuongeza ufaulu kwa wanafunzi wa kata ya Njia panda na kutumia nafasi hiyo kuaomba Wananchi kutoa ushirikiano pindi utakapohitajika.
Kwa upande wao wakazi wa kata ya Njia panda, Jesca Mzanaki alisema kuwa kitendo cha serikali kujenga shule ya sekondari ya kata ndani ya eneo la kata itasaidia Wanafunzi kukwepa vishawishi vilivyokuwa vikipelekea kukatisha masomo yao.
Naye Nuru Mohamedi aliomba serikali kuhakikisha inasimamia ujenzi huo ili uweze kukamilika mapema na ifikapo Januari mwakani shule hiyo ianze kupokea wanafunzi.
Mwisho…
0 Comments