WAKULIMA wa zao la korosho mkoani Pwani wanatarajia kupata kiasi cha shilingi bilioni 19.4 kutokana na mauzo ya korosho za msimu huu unaoendelea.
Hayo yalisemwa mjini Kibaha na mkuu wa mkoa wa Pwani Abubakari Kunenge alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake.
Kunenge alisema kuwa msimu huu mkoa unatarajia kuvuna zaidi ya mara mbili tofauti na mwaka jana ambapo mkoa uliweka nguvu ili wilaya zinazolima zao hilo ziongeze uzalishaji.
"Bei msimu huu imepanda kwani ni shilingi 2,040 kwa kilo ambapo mwaka jana ilikuwa 1,300 kwa daraja la kwanza na ilikuwa ni changamoto kupata daraja la kwanza,"alisema Kunenge.
Alisema kuwa hadi sasa fedha ambazo wakulima watapata ni za minada sita tu ambao ulifanyika Novemba 24 na bado minada inaendelea.
"Kwa kweli mwaka huu wakulima watapata fedha nyingi ambapo wengi walikata tamaana ya kulima zao hili na kuanza kulima mazao mengine lakini kwa bei kupanda itawavutia kuendelea kulima," alisema Kunenge.
Aidha alisema kuwa kwa upande wa zao la ufuta mavuno yatakuwa tani 11,940 toka tani 7,000 hivyo kuwa msimu mzuri kwa wakulima wa zao hilo kwenye mkoa wa Pwani.
"Haya ni mazao makubwa ya biashara kwenye .koa wetu tutaendelea kuwahamasisha wakulima walime kwa kufuata kanuni bora za kilimo na tutawapatia wataalamu na pembejeo za kilimo," alisema Kunenge.
Alibainisha kuwa kwa miaka iliyopita ilikuwa ni ngumu kupata korosho daraja la kwanza lakini mwaka huu imepatikana na bei ilivyokuwa inauzwa Mtwara na Pwani ndiyo hiyo hiyo.
Katika hatua nyingine aliwataka wakulima kutumia mvua zilizoanza kunyesha kwa kulima mazao yanayostawi kwa muda mfupi.
0 Comments