Katibu mkuu wa elimu,sayansi na teknolojia Dkt Leonard Akwilapo amewataka wahitimu wa chuo Cha ufundi Arusha kutumia taaluma zao kutatua changamoto zilizopo katika jamii na Taifa kwa ujumla.
Dkt Akwilapo aliyasema hayo katika mahafali ya 13 ya chuo Cha ufundi Arusha (ATC) ambapo aliwahimiza wahitimu hao kutumia taaluma na ujuzi waliopata kwa weledi na kujali maslahi mapana ya nchi pamoja na kufanya changamoto zilizopo katika jamii kuwa fursa na kuweza kuzitatua.
Aidha alisema kuwa wizara ya elimu na serikali kwa ujumla inatambua na kuthamini mchango mkubwa unaotolewa na chuo hicho katika kuzalisha wataalamu katika ngazi zote za elimu ya ufundi ndio maana serikali inakitumia chuo hicho katika miradi mbalimbali ya ujenzi na ukarabati wa majengo ya serikali na hiyo ni kutokana na kutambua uwezo, umahiri na uadilifu wao katika kusimamia miradi.
“Idara yangu imetumia utaalamu wenu katika kusimamia vyuo vya veta hapa nchini na kwakuzingatia ongezeko kubwa la wanafunzi wanaohitimu elimu ya msingi na sekondari ambapo serikali kupitia wizara ya elimu imejipanga kuimarisha vyuo vya ufundi na ufundi stadi hapa nchini,ikiwa ni pamoja na kuviwezesha kuwa na vifaa bora na vyakisasa vyakujifunzia na kufundishia,”alisema Dkt Akwilapo.
Alisema mpango huo utasaidia kuweza kuchukua wanafunzi wengi zaidi lakini pia kutoa elimu bora inayoendana na mabadiliko ya teknolojia na ushahidi wa Jambo hilo ni ukarabati uliofanyika katika chuo hicho ya kuboresha miundombinu ya kufundishia.
Kwa upande wake mwenyekiti wa bodi ya utawala wa chuo hicho Profesa Siza Tumbo ameishukuru serikali kwa kukiwezesha chuo kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazoathiri utekelezaji wa majukumu ya chuo kwa kuongeza bajeti ya chuo kila mwaka kwa ajili ya miradi ya maendeleo ili kuboresha miundombinu ya chuo hicho.
"Moja ya matunda ya juhudi hizo ni ujenzi wa bweni la wanafunzi wa kike lenye uwezo wa kulaza Wasichana 428 ambapo litakapokamilika litatusaidia kutatua kiasi kikubwa cha tatizo la uhaba wa malazi kwa wanafunzi hao,”alisema Profesa Tumbo.
Naye kaimu mkuu wa chuo hicho Dkt,Musa Chacha alisema kuwa kati ya wahitimu 952 wahitimu wa kike ni 189 sawa na asilimia 19.9 na wahitimu wa kiume wakiwa ni 763 sawa na asilimia 80.19 ambapo kumekuwa na ongezeko la asilimia 42.7ukilinganisha na wahitimu wahitimu mwaka wa masomo 2019/2020 ambao walikuwa 667,wakike 115 sawa na asilimia 26.4 na wakiume 321sawa na asilimia 73.6.
Alifafanua kuwa chuo kumekuwa na mafanikio katika nyanja za utafiti,ubadilishaji maarifa na huduma za kijamii pamoja na kuongeza rasilimali mbalimbali za uendelezaji wa miundombinu,ikiwa serikali imeendelea kugharamia na kuthamini mafunzo ya wafanyakazi wa kada mbalimbali na kuwapa stahiki zao mihimu za kiutumishi.





0 Comments