Mkurugenzi wa Shirika la Light for The World, Joseph Banzi amesema kuwa asilimia 70 ya watoto wenye ulemavu wa macho wanaosaidiwa na Shirika hilo kupitia katika mradi wa elimu wamefanya vizuri shule za msingi na kufanikiwa kuingia Sekondari.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam wakati akifungua mkutano wa siku mbili wa wadau wa elimu uliozishirikisha Taasisi mbalimbali zinazowasaidia watoto wenye ulemavu wa kuona amesema kuwa, miaka mitano ijayo watapeleka mradi huo katika shule za Sekondari Ili kuwaendeleza watoto hao.
"Kwa sasa tupo katika shule za msingi lakini miaka mitano ijayo tunajipanga kwenda shule za Sekondari maana watoto wetu wameshafika huko inabidi tuendelee kuwasaidia waweze kufanya vizuri katika masomo yao"amesema Banzi.
Aidha, amesema Mkutano huo utatoa matokeo chanya (fursa) kwani wataweza kujadili changamoto mbalimbali za watoto wenye ulemavu wa kuona, na kuzipatia ufumbuzi ambapo kila Taasisi itashiriki kutoa maoni yake katika kuwasaidia watoto hao.
Hata hivyo, amesema mradi huo umeshawafikia watoto 311 kutoka mikoa ya Morogoro na Dodoma ambapo wameweza kuwapatia vifaa mbalimbali vya kujisomea katika masomo yao.
Ameongeza kuwa, lengo la Mkutano huo ni kubadilishana uzoefu kulingana na changamoto za watoto wenye ulemavu na kuangalia namna ya kuwasaidia, huku akitaja changamoto zinazowakabili watoto hao ikiwemo kukosa matibabu pamoja na vifaa vya kuwasaidia kupata elimu..
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Shirikisho la Vyama vya Watu wenye Ulemavu (SHIVYAWATA), Ernest Kimaya, amesema tafiti zinaonyesha kuwa, changamoto bado zipo zinazowafanya watoto wenye ulemavu kushindwa kupata elimu licha ya kufanyika makomgamano mbalimbali ya kuweza kuwasaidia watoto hao.
"Changamoto zipo nyingi zinazowakwamisha watoto hawa kukosa elimu ikiwa ni pamoja na ukosefu wa walimu wenye taaluma ya ulemavu na vifaa vya kufundishia na kwamba kuna sera za kuwajumuisha wanafunzi wote kupata elimu hata walio na changamoto za ulemavu bila ya ubaguzi"amesema Kimaya.
Aidha, amesema kupitia Mkutano huo wanaangalia namna bora ya kuweza kuwasaidia watoto hao kupata elimu jumuishi, ambapo jamii ina nafasi kubwa ya kuhakikisha inawatambua watoto wenye changamoto ya ulemavu.
Hata hivyo, amesema watoto wenye ulemavu wa macho wamekua wakifungiwa ndani, na wengine wanaachwa nyumbani, hivyo, jamii inapaswa kupaza sauti zao kuwatetea Ili nao wapate haki zao za msingi kama watoto wengine.
0 Comments