ADELADIUS MAKWEGA-WUSM MBEYA
Maandalizi ya kilele cha Tuzo za Filamu Tanzania yamekamilika ambapo Kilele hicho kinafanyika Jioni ya leo Disemba 18, 2021 katika ukumbi wa Tughimbe mkoani Mbeya chini ya Usimamizi wa Bodi ya Filamu Tanzania.
Kilele hicho kilitoa nafasi kwa wasanii hao wanaoshiriki kunyakuwa tuzo hizo kutembelea vivutio mbalimbali vya kitalii mkoani Mbeya na Songwe.
Wakizungumza baadhi ya wasanii hao, wamesema kuwa kitendo cha Bodi ya Filamu kuandaa tuzo hiyo kinakuwa motisha kubwa na mwanga unaongeza nuru katika tasnia ya filamu nchini.
“Kwa kilele cha tuzo hizi za leo, anayeshinda atakuwa akitambulika kiserikali na zaidi ya hayo itajenga ushindani miongoni mwetu, binafsi naona sasa tunaelekea kufika katika ndoto niliyokuwa nikiiota wakati naingia katika sanaa” Alisema msanii Baby Madaha.
Jiji la Mbeya limeonekana likipambwa na sura za wasanii hao huku wakizunguka madukani na matembezi hayo ya wasanii yakiwavutia mno wakaazi wa jiji hili lililopo Nyanda za Juu Kusini mwa Tanzania.
Hali ya hewa ya Jiji hili ilikuwa ya nyuzi joto kati ya 17-18 sentigredi kwa majira ya mchana wakati asubuhi na mapambazuko yalipambwa na jua la kawaida ambalo lilitoweka majira ya mchana na kukaribisha mvua yaa manyunyu.
Kilele hicho kinatarajiwa kuhudhuriwa na Kamati ya Bodi ya Maendeleo ya Mfuko wa Sanaa nchini, viongozi kadhaa wa Mkoa wa Mbeya, Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii na watumishi na viongozi kadhaa wa Wizara ya Utamaduni Sanaa na Michezo ambao wapo Mbeya kwa sasa.





0 Comments