Kituo cha uwekezaji nchini(TIC)kimeitangazia Africa na dunia kwa ujumla kuwa Tanzania ni sehemu salama kwa shughuli za uwekezaji na kuwa milango ipo wazi kwa yeyote anayetaka kuja kuwekeza hususan katika sekta ya utalii.......Na Gift Mongi _Moshi Kilimanjaro
Mwakilishi wa kituo hicho Daud Riganda aliyasema hayo mara baada ya kushuka mlima Kilimanjaro katika maadhimisho ya miaka 60 ya Uhuru wa Tanganyika ambapo alikuwa ni miongoni mwa watu 150 waliopanda mlima huo kuanzia desemba 05 na kuongeza kuwa Tanzania ina sekta nyingi zinazofaa kwa uwekezaji hivyo milango ipo wazi.
Kwa mujibu wa Riganda ambaye pia ni meneja wa TIC Kanda ya Kaskazini ni kuwa rasilimali zote ambazo zinafaa kwa uwekezaji zinapatikana nchini tangu uhuru hadi Sasa na kuwa amani na utulivu ambavyo ni muhimu kwenye uwekezaji pia vipo kwani hakuna mwekezaji anayependa kuwekeza sehemu isiyo na utulivu au amani.
"Sisi TIC tumeadhimisha miaka hii 60 ya uhuru tukiwaambia wawekezaji kuwa Tanzania bado ni sehemu salama kwa kufanya shughuli za kiuwekezaji kwani rasilimali zipo pamoja na amani na utulivu ambavyo ndio vivutio muhimu"alisema Riganda
Alisema zipo sekta mbalimbali ambazo bado zinahitaji uwekezaji kama kilimo,uvuvi,viwanda vya kuongeza thamani,sekta ya utalii na miradi mbalimbali na kuwa bado kituo hicho kinahitaji wawekezaji hao kwani mazingira ni rafiki na yanaruhusu kwa kazi hizo.
"Tumekuwa na kauli mbiu ya kuwaita wawekezaji kuja katika ardhi ya Tanzania kuwekeza Tanzania kwani mazingira yanaruhusu na sio kwa wageni peke yake bali hata wazawa wanaruhusiwa vile vile kuwekeza kwenye miradi kadri watakavyoona inafaa"alisema
Kituo cha uwekezaji (TIC) kilianzishwa rasmi mwaka 1997 baada ya kupitishwa kwa sheria ya uwekezaji kimekuwa na dhima kuu ya kukuza uwekezaji ikiwa ni pamoja na kuhamasisha,kuratibu,na kuwezesha uwekezaji wenyewe sio tu kwa wageni bali hata kwa wazawa.
"Tunayo mambo mengi yakujivunia kama kituo katika hii miaka 60 ya Tanganyika tumechangia upatikanaji wa ajira,tumekuza mitaji lakini pia uwezo wa kuhudumia jamii katika sera ya kurudisha faida kwa jamii"alisema
Afisa habari na Uhusiano wa bodi ya utalii nchini(TTB) Augustina Makoye aliwapongeza wananchi kwa mwitiko mkubwa waliouonyesha kwa kujitokeza kwa wingi kuupanda mlima huo huku akiwahimiza kuendeleza ari hiyo katika kutembelea vivutio vingine vya utalii vilivyopo maeneo mbalimbali hapa nchini.
Safari hiyo iliyoandaliwa na shirika la hifadhi za Taifa, (TANAPA) kwa kushirikiana na kampuni ya uwakala wa utalii ya ZARA ilijumuisha watu kutoka taasisi mbalimbali za umma na binafsi ikiwemo TANAPA wenyewe, JWTZ, Bodi ya utalii nchini(TTB), Wakala wa Huduma za Misitu nchini,(TFS), Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro,(NCAA), Mamlaka ya Usimamizi wa wanyamapori, (TAWA), Benki ya NBC na waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali ndani na nje ya nchi.
0 Comments