MKUU wa Mkoa wa Ruvuma Brigedia Jenerali Wirbart Ibuge amewataka wafanyabiashara wa Mkoani humo kuwa wazalendo wa kulipa kodi na kuachana na tabia ya kukwepa kodi .......Na Amon Mtega,Songea.
Hayo ameyasema na mkuu huyo kwenye viwanja vya ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma wakati akigawa sukari mifuko 550 sawa na tani 11 ambayo ilikamatwa na mamlaka ya mapato (TRA) mkoani Ruvuma mwaka jana wilayani Mbinga mkoani humo
Ibuge amesema kuwa chanzo cha baadhi ya wafanyabiashara kukamatwa na bidhaa mbalimbali ikiwemo Sukari za magendo ni kutokana na wafanyabiashara hao kukosa uzalendo wa kutokulipa kodi jambo ambalo halikubaliki.
Amesema kuwa ili kukomesha vitendo vya watu kupitisha mali za magendo inatakiwa wananchi kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama wanatakiwa kuimarisha ulinzi kwenye mipaka ya nchi ikizingatiwa kuwa mkoa wa Ruvuma umepakana na Nchi mbili za Malawi na Msumbiji ambako bidhaa nyingi za magendo zinatokea huko na kusababisha ukwepaji wa kodi za Serikali.
“ Nachukua nafasi hii kumpongeza Meneja wa TRA na wafanyakazi wote wa mamlaka ya Mapato Tanzania kwa kushirikiana na vyombo vya usalama kwa namna wanavyofanya kazi kwa lengo la kuhakikisha kodi inapatikana na mnamlinda afya za mlaji kwa kuhakikisha chakula kinachopelekwa sokoni kisiwadhuru wenzetu” amesema Bridigadia Jenerali Ibuge
Kwa upande wake Meneja wa Mamlaka ya Mapato Tanzania Mkoani Ruvuma Amina Ndumbogani amesema kuwa mifuko 550 ambayo ni sawa na tani 11 zilikamatwa zikiwa zinaingizwa Nchini Tanzania kutoka nchi jirani ya Malawi kinyume cha sheria na taratibu za forodha.
Ndumbogani amesema kuwa sukari hiyo iliyokamatwa imegawiwa katika makundi maalumu kwenye Wilaya zote za Mkoa wa Ruvuma ambapo ameyataja makundi hayo kuwa ni Hospital, Magereza, vituo vya watoto yatima na wenye mazingira magumu na shule zenye wanafunzi wenye mahitaji maalumu
Ametoa wito kwa wafanyabiashara wote Nchini kuacha kufanya biashara ya kuingiza bidhaa Nchini bila kufuata sheria na taratibu za forodha na ushuru wa bidhaa ya mwaka 2004 na 2010 chini ya Jumuiya ya Afrika Mashariki kwani ukiukwaji wowote ule wa sheria za ukusanyaji wa mapato ya Serikali hupelekea kuikosesha Serikali mapato ambayo yangesaidia katika kuleta maendeleo ya nchi
Awali Mkuu wa Wilaya ya Songea Pololet Mgema akimkaribisha Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Brigedia Jenerali Wilbart Ibuge amesema kuwa matukio ya kukamatwa kwa bidhaa za magendo yanatokea mara kwa mara na hasa Ziwa Nyasa kupitia Mbambabay ambako inadaiwa kuna njia nyingi za panya ambapo alihimiza kuimarisha doria kwenye maeneo hayo
Mmoja ya wapokeaji wa msaada huo wa sukari akiwemo Mrakibu Mwandamizi wa Jeshi la Magereza Emmanuel Ndyuka ambaye pia ni Mkuu wa Gereza la Kilimo la Kitai amesema kuwa msaada huo kwao umewapa faraja sana na kwasababu jeshi hilo limekuwa likijiendesha vitu vingi tumekuwa tukivinunua, hivyo msaaada huo umetusaidia kupunguza baadhi ya matumizi ambayo tumekuwa tukiyafanya na kwamba msaada huu moja kwa moja utawasaidia wafungwa.
0 Comments