katibu mkuu wa wizara ya afya Profesa Abel Makubi amesema kuwa Serikali ina nia njema kutaka kuboresha afya za wananchi wake ili waendelee kuzalisha na kukua kiuchumi..
Prof Makubi aliyasema hayo wakati akiongea na wenyeviti wa serikali mtaa, vitongoji ,kidini , kamati ya ulinzi na Usalama na viongozi wengine katika kuelekea kwenye uzinduzi wa awamu ya pili wa mpango shirikishi na harakishi wa uhamasishji wa chanjo dhidi ya Uviko-19, itakayofanyika 22/12/2021.
Profesa Makubi amesema kuwa Serikali chini ya Rais Samia Sulluhu Hassan ina nia njema kwa wananchi wake na hivyo kuhakikisha Wananchi wanapata kinga na hivyo kufikia asilimia 60 ya kinga kwa muda mfupi.
"Hakuna chanjo iliyofanikiwa kwa kulazimisha bali kwa kuelimishana na wananchi na kuelewa sayansi , hivyo baadae mtu kuamua kuchanja Kwa hiari yake.
Aidha alisema kuwa kampeni hiyo ambayo itaenda kuwatumia viongozi wa mitaa wenyewe ambapo ni lazima wamilimiliki na kufanya wenyewe ndio maana wameamua kushusha kwa wananchi na wote kuwa timu moja mtaani.
Alifafanua, Kampeni ya mtaa Kwa mtaa, haileti ulazima bali ni kupeana elimu ngazi ya mtaa na Wananchi kwa hiari yao kwenda kuchanja .
Alisema licha ya kuchanja bado wananchi wanatakiwa kuendelea kuchukua tahadhari kwa kunawa mikono mara kwa mara na maji tiririka na sabuni,kuepuka misongamano na kuvaa barakoa.
"Jambo jingine niwakumbushe wananchi kufanya mazoezi pamoja na kula lishe bora,kwani mazoezi ni muhimu na inasaidia mifumo ya hewa kuwa mizuri"Alisisitiza Prof.Makubi
Naye, Katibu Mkuu kutoka Ofisi ya Rais-TAMISEMI Prof. Riziki Shemdoe amesema kuwa nchi inapoelekea kwenye sikukuu za mwisho wa mwaka wameona ni muhimu kushirikishana na viongozi wa dini,mitaa na kimila ili kuwa na namna bora ya kuwafikia wananchi ili kuweza kuwalinda wazee waliopo majumbani.
Prof Shemdoe hakusita kuwakumbusha viongozi hao kuendelea kuwaelimisha wananchi kuhusu umuhimu wa chanjo ya UVIKO-19 na kuendelea kuchukua tahadhari za kujikinga na ugonjwa huo.





0 Comments