Kaimu Afisa uhamasishaji Mpango wa Taifa wa damu salama Be. Lucas Migeto amesema kuwa Msimu wa sikukuu umekuwa na changamoto katika upande wa uchangiaji damu na kupelekea kupungua huku mahitaji ya damu wakati mwingine kuongezeka.
Akizungumza na Matukio Daima Lucas Migeto Kaimu Afisa Uhamasishaji mpango wa Taifa wa damu salama kanda ya Ziwa ameeleza kuwa wakati wa msimu wa sikukuu shule na vyuo karibu vyote hufungwa na wafanyakazi huwa likizo hivyo husababisha kupungua kwa idadi ya wachangiaji damu.
Lucas ameeleza kuwa kwa asilimia kubwa ya wachangiaji damu wanapatikana shule za sekondari, vyuo vya Elimu vya kati pamoja na vyuo vikuu.
Ameeleza kuwa mahitaji ya damu kwa mwaka 2021 ni chupa 550, 000 ambayo ni sawa na asilimia 1 ya idadi ya wananchi na malengo ya ukusanyaji wa chupa ni 375, 000 ambazo ni asilimia 70 ya mahitaji ya damu.
Lucas amesema kuwa mpango wa Taifa wa Damu salama haujaweza kufikia lengo la kukusanya chupa za damu ambazo zinakidhi mahitaji ya nchi nzima.
"Repoti ya mpango waTaifa wa Damu Salama inaonesha kwa kipindi cha mwaka 2019/2020 kwa kushirikiana na timu za halmashauri tumeweza kukusanya chupa za damu 312, 714 ambayo ni sawa na asilimia 57 ya mahitaji" alisema Lucas.
Ameeleza kuwa shirika la afya duniani linaelekeza kila mwanachama kukusanya damu asilimia 1 ya wakazi wa nchi yake au chupa 10 kwa kila wananchi 1000 ili kujitosheleza na mahitaji ya damu salama wakati wote na takwimu za mwaka 2019/2020 na kwa Tanzania umefikia chupa 6 kwa watu 1000.
Hata hivyo ameeleza kuwa malengo ya ukusanyaji wa damu chupa ni19, 514 nchi nzima huku kila timu inatakiwa kukusanya asilimia 3 ya malengo kwa mwaka.
Ameyataja baadhi ya makundi yenye uhitaji wa damu kwa asilimia kubwa ni pamoja na watoto chini ya umri wa miaka mitano (asilimia 42), wakina mama wakati wa kujifungua (asilimia 21) , wahanga wa ajali (asilimia 7) pamoja na wagonjwa wenye saratani, sikoseli virusi vya Ukimwi na makundi mengine( asilimia 30).
Aidha ametoa wito kwa wananchi kuendelea kujichangia damu hususani katika kipindi hiki cha msimu wa sikukuu ili kufika malengo na kuweza kusaidia wahitaji wa damu katika hospital.





0 Comments