Header Ads Widget

"NINAO UWEZO WA KUVAA 'VIATU' VYA MAALIM SEIF"HAMAD MASOUD HAMAD

Mtangaza nia ya kugombea Uenyekiti wa ACT-WAZALENDO, Hamad Masoud Hamad kushoto akizungumza na waadishi wa habari Dar es Salaam leo Desemba 1,2021.

Na Riziki Abdallah, Dar

FIlimbi imepulizwa tayari kuashiria kuanza mchuano wa mbio za nyika. 


Hivi ndivyo tunavyoweza kusema baada ya Mjumbe wa Kamati Kuu wa ACT Wazalendo, Hamad Masoud Hamad kutangaza nia ya kutaka kuvaa 'viatu' vya aliyekuwa Mwenyekiti wa chama hicho Taifa, marehemu Maalim Seif Sharif Hamad.


Hamad anakuwa mgombea wa kwanza kutangaza hadharani nia yake ya kutaka ridhaa ya kukiongoza chama hicho akichukua nafasi iliyoachwa wazi na Maalim Seif aliyefariki dunia Februari 17,2021.


Moja ya jambo ambalo ametaja kulivalia njuga akiwa Mwenyekiti wa ACT Wazalendo Taifa ni kuendeleza ajenda na msukumu wa kuifanya Zanzibar kuwa na Mamlaka kamili ili iweze kuendelea kiuchumi bila kuingiliwa na taasisi au upande wowote.


Akizungumza na waandishi wa habari leo Desemba 1,2021 Jijini Dar es Salaam, Hamad amesema kuwa amejipima na kuona  anatosha kumrithi Maalim Seif kutokana na alivyojengwa na kiongozi huyo tangu akiwa kijana.


Amesema amefanya kazi na Maalim Seif tangu kuanza kwa mfumo wa vyama vingi nchini mwaka 1992, akiwa kijana pekee kwenye Chama Cha Wananchi (CUF) kipindi hicho, hivyo uzoefu alionao unatosha kushika nafasi aliyotangaza kuiomba.


Masoud, ambaye amepata kuwa Waziri wa Miundombinu kwenye Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK), kabla ya kujiuzulu kutokana na ajali ya Meli ya Mv Spice Islanders, amesema anaamini katika siasa za ujenzi wa hoja na maridhiano kama ndiyo msingi wa amani na utulivu wa Wazanzibar wote.


“Ninaweza kuvaa viatu vya Maalim Seif, bila kuchechemea. Maalim ameniacha vizuri. Tofauti ya Maalim na mimi, ni jina, umri, ila nina uwezo wa kuongoza, ninafanana naye kwa hoja naamini katika maridhiano.


“Nimefanya kazi na Maalim takribani miaka 30, nilikuwa karibu naye tangu kuanzishwa kwa CUF, na ni kijana pekee niliyejitoa kufanya kazi na wazee hawa ambao wote walikuwa wakubwa kwangu, nimevuna mengi kutoka kwao.


“Siasa si nguvu ya ushindani, nikipata ridhaa, nitazingatia kutatua kero za wananchi, kujenga mtandao wa chama kilicho makini hususan Tanzania Bara ili kiwe na nguvu kama ilivyo Zanzibar." amesema Hamad.


Aidha  alisisitiza kuwa akichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa ACT Wazalendo Taifa ataanzisha dawati maalum la kusikiliza kero, kupambana na  sheria kandamizi zinazokiuka haki za binadamu ikiwamo kufanyia marekebisho sheria zote ambazo hazina maslahi mapana kwa Watanzania kwa ujumla wake.

Katika msisito huo pia amebainisha kuwa atasimamia na kudumisha Serikal atahakikisha chama chake kinajizatiti katika ngazi ya majimbo, mikoa na taifa na kubuni njia mbadala za kujipatia mapato ya kujiendesha.


“Tutashirikiana na vyama vingine, taasisi mbalimbali na wadu kuleta msukumo kuhakikisha upatikanaji wa Katiba mpya, na Tume huru ya Uchaguzi. Chama kitajidhatiti kuhakikisha hakiporwi ushindi wake kwenye Uchaguzi Mkuu na Serikali za Mitaa zijazo" amesema.


Mwisho.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI