Na Moses Ng’wat, Songwe.
Yaledi Sinkala (38), mkazi wa wilaya ya Momba, mkoani Songwe, amehukumiwa kifungo cha miaka 40 jela baada ya kupatikana na hatia ya kuzini na maharimu (ndugu) mwenye changamoto ya afya ya akili.
Hayo yamebainishwa Disemba 24, 2025 na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe, Augostino Senga, wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio ya jeshi hilo katika kudhibiti matukio ya uhalifu na uhalifu, pamoja na namna jeshi hilo lilivyojipanga kuimalisha ulinzi na usalama kuelekea sikukuu za mwisho wa mwaka.
Kamanda Senga alisema mtuhumiwa huyo baada ya kukamatwa na jeshi hilo na kufikishwa katika mahakamaya Wilaya hiyo, Novemba 18, 2025 alikutwa na hatia na kufungwa miaka 40.
Aidha, Kamanda Senga alibainisha kuwa kupitia oparesheni na mikakati hiyo ya kudhibiti uhalifu, Jeshi hilo limefanikiwa kuwafikisha mahakamani watuhumiwa wengine wawili kwa makosa mbalimbali, ambao pia wamehukumiwa vifungo vya muda mrefu.
Alifafanua kuwa watuhumiwa hao ni Nyati Kapongo (32), mkazi wa Wilaya ya Songwe, alikamatwa kwa tuhuma za kubaka na kufikishwa mahakamani Novemba 24, 2025, ambapo alihukumiwa kifungo cha miaka 30 jela baada ya mahakama kujiridhisha na ushahidi uliowasilishwa.
Alimtaja mtuhumiwa mwingine kuwa ni, Walless Mwamengo (45) ambaye alihukumiwa kifungo cha miaka 20 jela pamoja na faini ya shilingi milioni 7, Novemba 19, 2025, katika Mahakama ya Wilaya ya Songwe kwa kosa la uhujumu uchumi.
Akizungumzia suala la usalama kuelekea sikukuu za mwisho wa mwaka, Kamanda Senga alisema Jeshi la Polisi Mkoani humo limejipanga kikamilifu kudumisha amani na utulivu kwa kuimarisha ulinzi katika nyumba za ibada, maeneo ya mikusanyiko ya watu, viwanja vya michezo ya watoto, kumbi za starehe pamoja na makazi ya wananchi.
Aliongeza kuwa jeshi hilo litaendelea kufanya misako na doria za mara kwa mara kwa kutumia magari, pikipiki, askari wa miguu pamoja na mbwa wa polisi ili kuzuia na kudhibiti vitendo vya uhalifu katika mkoa mzima.
Kamanda Senga aliwataka wananchi kuendelea kushirikiana na Jeshi la Polisi kwa kutoa taarifa za uhalifu mapema, akisisitiza kuwa ushirikiano huo ni msingi muhimu wa kuhakikisha mkoa unaendelea kuwa salama wakati wote.






0 Comments