Header Ads Widget

MBUNGE ZUENA BUSHIRI AWATAKA WATUMISHI WA SERIKALI KUSIMAMIA FEDHA ZA MIRADI YA MAENDELEO KWA UMAKINI.

 


NA WILLIUM PAUL,  MOSHI. 

Mbunge wa viti maalum (CCM)  kupitia mkoa wa Kilimanjaro,  Zuena Bushiri amewataka watumishi wa serikali kuhakikisha fedha zinazotolewa na serikali kwa ajili ya miradi ya maendeleo ya wananchi zinatumika kama zilivyokusudiwa. 




Mbunge Zuena alitoa kauli hiyo jana wakati alipotembelea ujenzi wa zahanati ya Mabungo na jengo la mama na mtoto pamoja na kutembelea shule ya sekondari ya Mashingia na kujionea ujenzi wa madarasa matatu katika shule hiyo.



Alisema kuwa, lengo la serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hasani ni kuhakikisha kuwa, wananchi wanapata huduma karibu hali inayopelekea kutoa fedha nyingi kwa ajili ya ujenzi wa miradi mbalimbali.



"Serikali imekuwa ikileta fedha nyingi kwa ajili ya ujenzi wa miradi ya maendeleo na wasimamizi wa miradi hii ni nyie watumishi wa serikali hivyo mnajuku kubwa la kuhakikisha mnazisimamia fedha hizi kwa weledi na umakini mkubwa ili lengo lililokusudiwa litimie" alisema Zuena. 




Mbunge huyo aliwataka kuhakikisha miradi hiyo inakamilika kwa wakati pamoja na gharama zake kuendana na fedha zilizoletwa na serikali.





Kwa upande wake, Diwani wa kata ya Kirua Vunjo kusini,  Peter Meela alisema kuwa, kata hiyo ilipokea milioni 50 ambapo milioni 15 ni umaliziaji wa zahanati ya Mabungo na milioni 35 kwa ajili ya ujenzi wa jengo la mama na mtoto katika zahanati hiyo. 



Meela alisema kuwa,  kwa sasa zahanati hiyo imeshaanza kutoa huduma kwa wagonjwa wa nje huku ujenzi wa jengo la mama na mtoto ukifikia asilimia 90.


Alisema kuwa, kata hiyo pia ilipokea fedha milioni 80 zilizotokana na mapambano dhidi ya ugonjwa wa Uviko 19 kwa ajili ya ujenzi wa madarasa manne ambapo shule ya sekondari ya Mashingia ilipata madarasa matatu na Uparo darasa moja hali ambayo itasaidia kupunguza tatizo la uhaba wa madarasa katika shule hizo. 




"Katika kata yetu kulingana na idadi ya wananchi tunauhitaji wa shule mbili za sekondari hali ambayo itasaidia kuondoa changamoto ya wanafunzi kutembea umbali mrefu kufuata shule pia tunauhitaji wa shule ya sekondari moja yenye kidato cha tano na sita" alisema Meela.




Mbunge huyo pia alikabidhi mchango wake wa matofali kwa ajili ya ujenzi wa nyumba ya Katibu wa umoja wa wanawake wa chama cha mapinduzi (UWT)  wilaya ya Moshi vijijini. 






Mwisho... 

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI