Disemba 4, 2021 nilikuwa nikifanya marekebisho ya chumba changu ninachokaa maana mvua zimeshaanza kunyesha katika mikoa mingine ya Tanzania, huku Dodoma zikiwa zinaonesha dalili hiyo. Maana mara zote mvua zinaponyesha mambo yanakuwa magumu juu ya hamisha hamisha ya kitanda na kukigeuza kukwepa matone ya mvua yasiingie ndani ya chumba changu..........ADELADIUS MAKWEGA _CHAMWINO
Kwa hiyo nilijulishwa kuwa kazi hiyo anaweza kuifanya vizuri fundi mmoja anayefahamika kama Ngosha. nilidamkia kwa ndugu huyu ambaye nilimkuta bado amelala. nikapiga hodi niiliitikiwa na sauti ya mama ambaye kwa mlio wa matamshi yake nilibaini kuwa alikuwa mdala wa Chigogo(mwanamke wa Kigogo). Mama huyu alinikaribisha, nikamuuliza hapa ndiyo nyumbani kwa Ngosha alinijibu ni kweli, Nikauliza yupo? mama huyu alinijibu kuwa ni kweli yupo, ngoja nikamuamshe.
Alipotoka (Ngosha) alikarikaribisha huku akiniambia kuwa hapa ndiyo kwangu, nikamuuleza tukakubaliana kuwa kazi hiyo itafanyika kwa shilingi 15,000/-.Kweli tulienda mguu kwa mguu mpaka kwangu na Fundi Ngosha kuianza kazi hiyo akiwa na msaidizi wake. Kazi ilifanywa ilipofika saa sita nilichemsha viazi vya mviringo na maharage nikala na mafundi hawa.
nikiwambia kuwa jamani hapa hakuna mwanamke wa kuwapikia vizuri kwahiyo tulikula pamoja viazi hivyo ili wao waendelea na kazi.Tulipomaliza kula kijana Saidia fundi aliuliza saa kwa kuwa simu yake iliingia katika maji na kioo cha simu hii hakioneshi, nilimjibu, akisema kuwa anataka kuwahi msikitini. Baada ya dakika kadha ilisikika azana nadhani kijana huyu saidia fundi aliwahi huko msikitini.
Ngosha aliendelea kujenga huku akikata vipande vya tofari mwenyewe, mimi nllitoka kidogo nikaenda kukaa upande wa pili kwenye benchi huku nikiwa nikafungua Youtube na kucheza wimbo wa Mshukuruni Bwana ni kutoka katika Old Swahili Catholic Hyms.
“Nani awezaye kuyanena matendo makuu ya Bwana-Aleluuya, kuzihubiri sifa zote, Aleluuya. Mshukuruni Bwana kwani ni mwema, Aleluuya, fadhili zake za dumu, milele Aleluuuyaa.”
Nikiwa nausikiliza wimbo huo ndugu Ngosha aliniambia kaka naona unanikumbusha Jumapili. Nikajibu kumbee! Akasema sana.Nikamuuliza kwanini?
“Unajua nilipoamia Chamwino Ikulu jamaa wakataka kunichagua kuwa Katibu wa Jumuiya lakini nikawaomba kama wanataka ushauri nitautoa, lakini uongozi kidogo kwa sasa wanisamehe.” Alisema Fundi Ngosha
Nikamuuliza inakuwaje tena unakataa uongozi wa dini, utaikosa pepo kaka? Ngosha alijibu kuwa ni kweli masuala ya uongozi mara nyingi yanahitaji utashi mkubwa wa yule anayechaguliwa kuwa kiongozi wa kundi hilo.
Ngosha akasema kuwa yeye kabla ya kufika Chamwino Ikulu alitokea Kitongoji cha Igudija, kijiji cha Kitumba, Kata ya Kisesa, Tarafa ya Kisesa Wilaya ya Magu Mkoa wa Mwanza. Anasema kuwa akiwa Magu alikuwa Katibu wa Jumuiya moja ya kanisa Katoliki. Siku moja kulikuwa na mfululizo wa misiba katika kjjiji hicho ambapo ndani ya mwezi mmoja kulitokea vifo vya wanafunzi wane waliokuwa wakisoma shule za sekondari na kila wiki alikuwa anakufa mwanafunzi mmoja. Msiba wa kwanza ukapita salama, wapi pili hivyo hivyo na watatu pia na sasa ukatokea misiba wanne.(Nikiwa nasimuliwa hayo saidia fundi alirudi kutoka msikitini-Ngosha akimuuliza kama na sisi ametuombea?)
Ngosha aliendelea kunisimulia kuwa siku ya kuzika msiba wa nne, kulikuwa na simanzi maradufu maana wazazi walikuwa wanawategemea watoto wao wanaosoma pale wakimaliza shule ili waweze kundelea na shule ili waje kupata kazi kuokoa familia zao, lakini Mungu amewachukua.Sasa kila mwenye mtoto shuleni hapo akiwa na shaka pengine baada ya msiba huo itakuwa msiba kwa mwingine.
Kila mmoja kijijini akijiuliza shida ni nini? Msiba ukiwa nyumba alifika Padri akasalisha ibada ya mazsihi na mara baaada ya kwisha watu waliaga, sasa ukafika wakati wa kuubena mwili kuelekea makaburini. Kabla ya kuubeba mwili huo, Ngosha kama katibu alikuwa bize na kukusanya michango ambayo ingesomwa makaburini. Ilisikika sauti ya juu ya jamaa mmoja aliyesimama na kusema.
“Jamani sasa tumechoshwa na tabia hii ya kufariki watoto wadogo, sasa mimi leo nasema hivi, msiba huu wa leo watazika wanawake.”
Kauli hiyo ilikuwa nzito hapa msibani watu wote kimya, kweli wanawake wakaanza kulibeba jeneza hilo kuelekea makaburini. Jamaa huyu aliyetamka maneno haya alikuwa anaitwa Maliganya, ambaye alikuwa kamanda wa sungusung wa kijiji. Kauli ya Maliganya ilitokana na wazo kuwa wanafunzi hao walikuwa wakifariki kwa kulogwa na wenye wivu.
Kwa utaratibu wa Wasukuma wazikaji tangu enzi ni wanaume. Siku hiyo tangu nyumbani hadi makaburini jeneza hilo likabebwa na wanawake. Jambo hilo ni mwiko lakini mwiko huo sasa unavunjwa kwa kuwa watoto wa watu wanakufa hovyo kijijini wakiwa wadogo. Mwili ulipofika makaburini kwa kuwa alikuwepo Padri alimwomba Maliganya kuwa wanaume washiriki kuzika na kweli alipokubali ndipo wanaume walishiriki.
Ngosha huku akijenga akaniambia kuwa tangu ulipotokea msiba huo na kutokana na tukio hilo hakukuwahi tena kufa mwanafunzi wa shule hadi yeye anaondoka kuja Chamwino huku wanafunzi wakisoma na kumaliza shule vizuri.
Fundi Ngosha anasema kuwa Ndugu Malinganya alikuwa ni kiongozi wa sungusungu huku akiwa na utashi wa kutatua kero za ndugu zake na huku akiheshimika mno na kila mtu kijijini hata Wilayani Magu.
Ngosha anasema kuna siku nyengine mama mmoja ambaye alikuwa na watoto aliiba mahindi kwa jirani yake, mama alikamatwa na umati wa watu wakitaka kumuua. Alipofika Maliganya alimshika mkono mama huyu na kumuokoa na kumwambia kwanza, mama huyu ameiba kwa kuwa kuna mwanaume mmoja miongoni mwetu hapa hajatekeleza majukumu yake ipasavyo. Kosa la Mama huyu ni kutofika kwa viongozi na kama angefika jambo hili lingeisha.
Sasa Kamanda wa Sungusungu Maliganya alimuita mkewe kwa jina la mtoto wake Mama Mashiku? Mama huyu aliitika Labeka! Maliganya akasema nenda nyumbani ukachukue debe la mahindi uje nalo hapa sasa hivi. Mke wa Maliganya alirudi na debe la mahindi akamkabidhi mama mwizi, Lakini Maliganya akaamua mama huyu kucharazwa viboko vitano hadharani.
Kweli mama alicharazwa bakora na kurudi nyumbani kwake. Swali ni je kama umma ule ungemmaliza mama yule ingekuwaje? Kamanda wa Sungusungu Maliganya aliokoa uhai wa mama yule.
Ndugu Ngosha anasema kuwa Maliganya ni kiongozo mwenye utashi ambayo sifa hii ni viongozi wachache wamebarikiwa kuwa nayo. Watu kila mara wanamwambia Maliganya agombee udiwani huku wakimchukulia fomu lakini hataki. Wengine wakitaka awe Mbunge wao lakini kamanda Maliganya yeye ameridhika tu na ukamanda wake wa Sungusungu wa Kijiji.
Ngosha anasema kuwa kuna siku aliwahi kusimuliwa na Maliganya akimwambia kuwa alipokuwa mdogo alikuwa akifanya kazi ya kuchimba mizizi ya dawa ya babu yake aliyekuwa mganga wa kienyeji na hata babu yake alipofariki aliacha wosia kuwa Maliganya asipatiwe mgao wa nguo za babu yake na pia alitakiwa kutokuoga siku 30 baada ya msiba huo.Wengi wakiamini kuwa Maliganya nazo nguvu za ziada lakini Ngosha anasema kuwa Maliganya ni Kiongozi mwenye utashi wa kuisadia jamii yake tu na wala si uganga, mali au chochote kile.Akisema watu wanamuitikia na wanampenda.
Kweli sasa ilikuwa saa 9 nilimuaga fundi Ngosha na yeye akiendelea na kazi na mimi kuwahi stendi ya njiapanda ya Chamwino Ikulu-Buigiri Kuelekea Dar es Salaam.
makwadeladius@gmail.com
0717649257
0 Comments