Kulingana waraka nambari 3 wa mwaka 2016 wa utoaji wa elimu ya msingi bila malipo umeyataja majukumu ya Wizara ya Elimu na TAMISEMI na kuzipachikia majukumu ambayo kwa jumla ni majukumu 13, majukumu sita kwa Wizara ya Elimu na saba ya TAMISEMI.
Nikianza na Wizara ya Elimu katika jukumu la kwanza kwa mujibu wa waraka huu ni kutoa nyaraka za mambo ya kuzingatia katika utekelezaji wa Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 katika utoaji wa Elimu ya Msingi bila malipo. Jukumu hili japokuwa ni jukumu la kwanza ni jambo jepesi kwa kuwa ni kuandaa tu maandishi hayo na kuyatawanya kwa wadau, ambao wametajwa katika waraka huu ambao ni TAMISEMI, Sekretarieti za Mikoa, Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi wa Halmashauri, Wakuu wa shule, Bodi/Kamati za shule, Walimu, Wazazi/Walezi, Wanafunzi na Viongozi wa Vijiji/Mitaa.
Kipengele cha pili kwa mujibu wa waraka huu ni kuwa kutenga pesa za utayarishaji wa mitihani ya kitaifa kulingana na wanafunzi waliopo katika shule za serikali. Hili pia ni jambo linalofanyika vizuri kwa kuwa hakuna hata mwaka mmoja tangu tamko la elimu bure kusikia kuwa kuna wanafunzi hawakufanya huo mtihani kwa kutolipa gharama za mitihani. Kwa maoni yangu kazi hii japokuwa inafanyika vizuri lakini ni dhana ya kibaguzi wa kuwatenga wanafunzi ambao hawasomi shule za umma. Hawa wote ni Watanzania wanaolipa kodi iwe wao wenyewe wazazi/ walezi wao. Kwa hiyo shule binafsi hawapaswi kulipia gharama za mitihani hiyo na Wizara ya Elimu itenge pesa kwa watoto wote wa Kitanzania.
Wazazi wanaopeleka watoto wao shule binafsi kiukweli wanaipunguzia serikalia yetu gharama kubwa ya kuwasomesha watoto wao wenyewe lakini ni wajibu wa serikali kuwalipia gharama za mtihani hiyo hilo linaonesha uwajibikaji wa serikali kwa wanafunzi wetu.
“Japokuwa baba alikuwa analipa ada yangu ya shule lakini nimefaidi matunda ya uhuru kwani mitihani yote tangu darasa la nne, darasa la sana, kidato cha pili, kidato cha nne na cha sita serikali yetu inalipia.” Msomo huyu analipiwa na Wazazi/ walezi wake anaweza kujinasibu. Hii pia inaijengea heshima serikali kwa watu wake wawe matajiri na hata masikini.
Tatu, Wizara ya Elimu kwa mujibu wa Waraka huu inawajibu wa kutenga fedha kwa ajili ya udhibiti ubora wa shule. Hapa pana shida kubwa, kwanza ofisi karibu zote za udhibiti ubora wa shule hazipo au wamekuwa wakijishikiza aidha kwa wakuu wa wilaya au kwa Halmashauri pia hawana vitendea kazi bora na vya kisasa. Kuna maeneo wanayo magari ambayo hayafanyiwi service yakiwa na hali mbaya kwa hiyo wanashindwa kufanya kazi yao vizuri ya kupitia katika shule za msingi na sekondari ili kukagua mazingira ya shule na namna elimu hiyo inavyotolewa.
Wengi wao wanashinda ofisini tu na mara moja moja wakipata mafuta kwa kuomba kwa taasisi zingine ndiyo wanafanya ukaguzi huo. Kazi yao mara nyingi kwa sasa wanayokuwa wakiifanya vizuri ni pale wakipangwa kusimamia mitihani ya kitaifa tu iwe ya darasa la nne, saba, kidato cha pili, kidato cha nne, na kidato cha sita. Ushauri wangu katika hili Wizara ya Elimu iwapeleke wadhibiti ubora wa elimu TAMISEMI kwa kuwa hawa wana shule, na hilo litakuwa jambo jepesi kwani ushauri wa wadhibiti ubora wa elimu kufanyiwa kazi kwa kuwa watakuwa wakiingia katika vikao vya Baraza la Madiwani na watakuwa sehemu ya idara ya halmashauri.
Kwa wale wadhibiti ubora wanaopata nafasi wamekuwa wakifanya kazi hiyo kwa shida na kuandika maoni na kuwapa nakala Mkurungezi, Mkuu wa Wilaya, Katibu Tawala na Wizara ya Elimu ambapo Wizara ya Elimu hawana shule.Ushauri wao mwingi mimi nauhita ni kama vile barua ya wasomaji katika gazeti. Kwa hili maoni na ushauri wao kufanyiwa kazi wawe sehemu ya TAMISEMI tu na wapatiwe pesa za kutosha na vitendea kazi wataifanya kazi yao vizuri.
Jukumu la nne kulingana na waraka huu ni kutenga fedha za ufuatiliaji na kuchukua hatua stahiki pale inapobidi. Hapa hakuna kinachofanyika kwa kuwa wizara inawategemea wadhibiti ubora wa elimu katika hili. Mathalani wadhibiti Ubora wamebaini kuwa kuwa katika shule A kuna tatizo mazingira ya shule hiyo hayafai kujifunzia ushauri utapelekwa Wizarani, wizara ya elimu ndiyo wataandika barua hadi TAMISEMI ndipo iwafikie wahusika, tena huo utakuwa ni kilichobainika tu. Je shida hiyo inawangoja wao? Suala la elimu lisipofanyiwa maamuzi haraka, maana yake madhara yake yataonekana baada ya miaka saba, minne au miwili. Masuala ya elimu yote maamuzi yake yanapaswa kufanyika kwa wakati. Ushauri kwa jukumu la nne ni kuwa kama ule wa jukumu la tatu.
Ndiyo kusema Wizara ya Elimu isishugulikie chochote kile juu ya Elimu ya awali, msingi na sekondari bali yenyewe ishughulikie elimu za vyuo na vyuo vikuu tu. Kwa kuwa majukumu yake mengi kwa waraka huu ni ya jumla na ya juu juu ndiyo maana sasa wanakuja na matamko ambayo yanaingilia majukumu ya wadau wengine kwa mujibu wa waraka huu wa elimu bure nambari 3, wa mwaka 2016.
Kwa leo naweka kalamu yangu chini huku bado nabubujikwa na machozi juu ya katazo la masomo ya ziada. Nasema katazo hilo halina tija yoyote kwa elimu ya taifa letu. Nakutakia siku njema.
makwadeladius@gmail.com
0717649257
0 Comments