Header Ads Widget

JE UTAKWENDA KUITUMIKIA JAMHURI YA KENYA?

 




Nilipofika Isimani -Tarafani nilibaini kuwa Kijiji cha Ujamaa Isimani kilikuwa maarufu sana kwa kilimo cha mahindi tangu Ujamaa. Nilibaini pia Wilaya ya Iringa Vijijini ilikuwa na pande mbili upande wa kwanza ulikuwa ukianzia maeneo ya isimani kwenda hadi Mtera unaokaliwa na makabila mchanganyiko wakiwamo Wagogo na Wamasai (wakulima na wafugaji), Wakisi, Wandendeule, Wamatengo na jamii nyengine ya Wangoni na Wahehe wachache (wakulima na wavuvi) Wandendeule, Wakisi na Wamatengo ambao hawa walihamia huko kwa kuwa wao ni wavuvi wakifanya kazi hizo katika Bwawa la Mtera........ADELADIUS MAKWEGA UWJ-BEN MKAPA.


Upande wa pili wa Wilaya hii ulikuwa ule unaopakana na wilaya nyengine za Mkoa wa Iringa ambapo huku kulikuwa na jamii ya Wahehe na Wabena(wakulima) wengi wakilima mahindi na mpunga. Huku ndiyo jamii iliyo kidogo jirani na maeneo ya Iringa Mjini na jirani na makaazi ya Chifu Mkwawa ambapo huko ndipo nyumbani kwa mheshimiwa  Wiliam Lukuvi. Mchanganyiko huu wa makabila niliuona hata darasani nilipokuwa nikifundisha kwani niliyaona majina hayo hasa ya Wakisi, Wandendeule na Wamatengo nilipowauliza wanafunzi walisema kuwa babu/babu alikuja kuvua samaki, baba alikuja kulima maana ardhi ya huku inarutuba sana.


Nilibaini kuwa japokuwa Mheshimiwa Lukuvi alikuwa hazaliwi ukanda huu wa Isimani-Mtera lakini miradi ya maendeleo ilipelekwa bila ubaguzi kwa mfano shule kubwa za sekondari za umma zilikuwa upande huu, huku zikiwa na mabweni ya wanafunzi wa kike kwa wakiume.


Serikali ya kijiji Isimani walinikabidhi nyumba ya kuishi ambayo nilibaini kuwa hapo kulikuwa na mchwa wengi. Nilibaini hata wakati wa kutayarisha mashamba wakulima hawakuwa na kazi kubwa kwani mabua na miti yote wakati wa kiangazi inatafunwa vizuri na mchwa. Hata mahindi yanastawi sana kwa kuwa mabua ya mahindi ukiacha shambani baada ya muda haukuti kitu kwa kuwa waheshimiwa mchwa huwa wameshafanya kazi yao vizuri. 


Nyumba hii ya kijiji nilikuwa nakaa na dada yangu mmoja ambaye alikuwa akifahamika kama Keti (muuza pombe). Nyumba hii iliyokuwa na vyumba vinne, sebule, jiko, stoo na choo huku ikiwa imezungushiwa ukuta. Dada yangu Keti alikuwa akinunua pombe huko inapopikwa anahifadhi ndani ya nyumba hii jioni anakwenda kuuza kijijini. Dada huyu alikuwa akiuza pombe zote halali na haramu.


Nikiwa kijijini nilipata rafiki yangu mmoja ambaye alikuwa mpiga picha alifahamika kama Mtisi (mpiga picha) huku akinipa habari tele za kijiji hiki. Rafiki yangu huyu alinijulisha kuwa nyumba hiyo niliyokuwa naishi ilijengwa kwa watumishi wa kijiji hicho lakini nyumba zilikuwa za kutosha na ndiyo maana nyumba hiyo walimpangishia Keti angalau kuifanyia usafi tu na isiharibike.


Kutoka kjijini hadi shule ulikuwa mwendo wa dakika 20 kwa mguuu, kwa kuwa nilikuwa na baiskeli niliyopewa na mbunge wa Isimani mheshimiwa Lukuvi ilisaidia mno kupunguza muda na nguvu za kutembea kwa miguu.


Nikiwa katika nyumba hii ya kijiji, dada Kate, muuza pombe, alinifundisha jambo moja kubwa kuhusu kupika kwa kutumia kuni chache.


“Mwalimu kwa kuwa unatumia muda mwingi kazini, unapopika maharage, washa kuni zako jikoni, bandika chungu katika jiko, weka maji katika chungu hicho, weka maharage makavu, juu ya chungu hicho weka chungu kingine jaza maji mengi. Alafu nenda zako kazini. Ukirudi saa nane utayakuta yameiva, unga maharage yako, pika zako ugali urudi tena kazini.” 


Somo hilo nalikumbuka hadi kesho kwani hadi sasa nawafundisha mabinti zangu ili waweze kupika maharage bila ya kutumia kuni/mkaa mwingi.


Nikiwa Isimani, kuna rafiki yangu mmoja ambaye nilisoma naye ualimu na yeye alipangiwa Iringa Vijijini kata nyengine alifika kunitembelea Isimani akiniambia kuwa kule alipo hali ni mbaya, ndugu huyu alinilalamikia kuwa kwake anazungukwa na wafugaji wa nguruwe sasa yeye ni ustadhi yaani anapata tabu sana. Ndugu huyu alikuwa akitokea Mafia na mimi nilimfahamu tangu tukiwa wadogo kwani wazazi wetu walikuwa pamoja huko Kilindoni-Mafia.


“Mimi nimekuja kukuaga, maana ninarudi Mkuranga nikafundishe hata shule binafsi maana naona mambo yamenishinda.”

Nilimshauri ndugu huyu kuwa haya ni ya kawaida tu, nguruwe ni nyama kaka. Baki huku tafuta binti uoe maisha yanaenda kama kawaida kaka. Nilitoa ushauri wangu. Ushauri huo ulikuwa sawa na mtu anayemlisha mtoto aliyezaliwa leo ugali na maharage. Kumbe ndugu yangu huyu alipokuja kwagu, mabegi yake aliyaacha Iringa Mjini.Kesho yake alipotoka kwangu alienda Mkuranga kufundisha shule ya binafsi.


Mimi nilibaki Iringa Vijijini, Kwa kuwa ilikuwa na ajira ya serikali mzee wangu aliniambia kuwa nikiwa huko Iringa nisitafute mchumba kwani kama nitatafuta mchumba huko nitashindwa kurudi nyumbani kuwasalimia ndugu, pia alisema kuwa mimi bado kijana mdogo sana.


Kwa utaratibu wa mila za kipogoro posa huwa inalipwa na baba, kama wewe ni baba na una watoto wa kiume watano basi unawajibu wa kuhakikisha ukiwa hai au umekufa huku nyuma unaanda mazingira ya watoto wako kuoa. Wapogoro, baba ndiye mlipa posa ya mtoto wake wa kiume. Kwa hiyo baba akisema sasa si wakati wa kuoa tambua kuwa hilo halina mjadala. Kumbuka wapogoro wanafanya hivyo kwa kuwa mtoto ni mali ya familia ya kiume na mtoto anachukua ukoo kwa baba.


Hata kama kijana wa Kipogoro akimkurupusha binti wa mtu na kumuweka ndani bila ya kibali cha baba tambua kuwa huyu hatambuliki hadi posa alipe baba/ baba mdogo au kaka mkubwa au babu kama hao wote hawapo.


Maelekezo ya mzee niliyasikiliza sana hata kama niliwaona warembe wa Iringa Vijijini, Dada zake mheshimiwa Lukuvi nilibaki tu moyoni kwa kuwatazama kwa macho, japokuwa nilikaa miaka zaidi ya mitano huko.


Nikiwa bado nipo Isimani, mzee huyu aliniambia kuwa kwanza mimi bado nina elimu ndogo nitafuta chuo cha kusoma atanilipia ada. Kweli kutekeleza agizo la baba nilitafuta chuo na nilipata Chuo Kikuu cha Tumaini Iringa.


Chuoni hapo sikupata kozi ya Ualimu bali Shahada ya Sanaa ya Habari.Hapo nilikutana na Afisa Usajiri wa chuo wakati huo Dkt. Irene Mkini alinitazama akaniambia kuwa kwanini usisome Shahada ya Sanaa ya habari? Nikauliza kwanini? Alinijibu kuwa kama ninavyokuona itapendeza sana kuwa mwanahabari.



Nilipokea ushauri huo lakini nikawa najiuliza kama nitasoma kozi hiyo maana kule jamaa wa elimu watasimamisha mshahara wao. Kwa hiyo nilipotoka hapo nilipomjulisha mwajiri alisema kuwa utaratibu wa ruhusa ya mwalimu kusoma ni lazima kusoma kozi inayohusiana na ulimu na uwe umefundisha zaidi ya miaka miwili kinyume na hapo basi acha kazi.


Nilirudi chuo kikuu kuendelea na masomo huku nikibaini kuwa wapo wanafunzi wengi ambao ni walimu walikuwa vyuo vikuu wakisoma masomo tafauti na ualimu na kazi wakiendelea nayo vizuri.


Nikiwa tayari nimelipa ada, kuna rafiki yangu mmoja ambaye alisomeshwa na Madaam Margaret Sitta Forodhani sekondari akisema sasa yeye ndiye Waziri wa Elimu twende tukamuone.


Margareth Sitta Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi wakati huo kabla ya kuwa mbunge aliwahi kufanya kazi na vyama vya wafanyakazi, aliwahi kuwa Afisa Elimu katika Wilaya mbalimbali, kwa wale waliowahi kusoma Azania na Forodhani miaka kati ya 1990-1999 watamkumbuka mwlaimu wao.


Mheshimiwa huyu ambaye alikuwa akisimamia vizuri maslahi ya elimu na walimu wanyonge kama walivyoniambia walimu wezangu niliamua kumfuata ofisini kwake magogoni Dar es Salaam. Lakini pia nikimfuata mwalimu wangu, je mwalimu wangu huyu atakuwa amebadilika tabia au mzimu wa cheo utakuwa umezidi kimo?


Nilipofika hapo nilikutana na na wasaidizi wa ofisi yake na kupewa nafasi ya kuzungumza naye huku akimuita Mkurugenzi wa Mafunzo wa wizara hii akimuekeza huyu mwalimu anataka kwenda kusoma, naona mmenyima ruhusa, kwani akienda kusoma na kumaliza hayo mafunzo atakwenda kuitumikia Jamhuri ya Kenya? 


Jamaa aliyeulizwa hakuwa na majibu, Mama Margareth Sitta aliniuliza mimi eti mwalimu ukimaliza masomo yako ya Uandishi wa Habari, utakwenda kuitumikia Jamhuri ya Watu wa Kenya? Jibu langu lilikuwa, hapana, Mheshimiwa. Basi mama Margareth Sitta alimuagiza Katibu Mkuu muda ule ule akiwa kando, kunipatia barua ya ruhusa masomoni (Release letter) ambayo nilipata siku hiyo na mimi nikitoka kwa vigelegele.


Je, mwanakwetu naitumikia Jamhuri ya Watu wa Kenya? Tunaitumikia Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa sasa. Kwa leo ebu niishie hapa, niendelee na kazi yangu hapa Uwanja-Benjamini Mkapa.


Makwadeladius @gmail.com

0717649257

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI