Header Ads Widget

HITIMA YA MIGOGORO YA ARDHI

 





Muundo wa Baraza la Ardhi na Nyumba la Wilaya Baraza hili ni miongoni mwa vyombo vya utatuzi wa migogoro ya ardhi Tanzania. Baraza la Ardhi na Nyumba la Wilaya huwa linaundwa na Waziri mwenye dhamana ya masuala ya Ardhi. Kwa mujibu wa sheria, linaweza kuundwa katika ngazi ya Wilaya, Mkoa au Kanda kutegemeana na wingi wa migogoro ya ardhi na nyumba kwenye eneo husika.


Muundo wa Baraza: Baraza hili litaongozwa na Mwenyekiti wa Baraza ambaye kwa mujibu wa Sheria lazima awe Mwanasheria, na atateuliwa na Waziri mwenye dhamana ya ardhi, na kuapishwa na Mkuu wa Mkoa. Mwenyekiti atashika wadhifa huo kwa muda wa miaka 3 na anaweza kuteuliwa tena baada ya muda huo. Kazi za Mwenyekiti ni pamoja na kusikiliza na kutolea uamuzi migogoro ya ardhi itakayoletwa mbele ya Baraza akishauriana na wajumbe wa Baraza. 


Baraza la Ardhi na Nyumba la Wilaya, kwa mujibu wa Sheria Na.2 ya mwaka 2002 lina wasaidizi wasiozidi saba (7) na watatu (3) kati yao, lazima wawe wanawake. Wasaidizi hawa huteuliwa na Waziri mwenye dhamana ya masuala ya ardhi kwa wakati huo kutokana na mapendekezo ya Mkuu wa Mkoa na lazima watoke katika eneo la Wilaya husika. 


Sifa za Wasaidizi wa Baraza la Ardhi na Nyumba la Wilaya. Awe raia wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mwenye akili timamu. Mkazi wa kudumu wa wilaya husika. Mwenye umri usiopungua miaka 21. Ambaye hajawahi kutiwa hatiani kwa makosa ya jinai hususani ya kufanya vurugu, kukosa uaminifu au tabia mbaya. Asiwe mbunge, diwani, mjumbe wa Halmashauri ya Kijiji, mjumbe wa Baraza la Ardhi la Kijiji au Baraza la Kata. 15.


Ukomo wa mamlaka ya Baraza la Ardhi na Nyumba la Wilaya Baraza lina ukomo wa aina mbili katika kufanya kazi zake. Ukomo wa Kieneo: Baraza lina uwezo wa kushugulikia migogoro ya mali au ardhi iliyopo katika wilaya, mkoa au kanda kutegemea mahali baraza limeundwa na kutekeleza shughuli zake kieneo. Ukomo wa kifedha: Baraza lina uwezo wa kusikiliza kesi za urejeshaji mali isiyohamishika yenye thamani isiyozidi shilingi milioni Hamisini (50,000,000) na mali inayohamishika isiyozidi thamani ya shilingi milioni Arobaini (40,000,000).


Majukumu ya Baraza la Ardhi na Nyumba la Wilaya ni kupokea ushahidi wa ziada kama utakuwa umeletwa, kuangalia kumbukumbu za maamuzi yaliyofanywa na Baraza la Kata, kufanya uchunguzi itakapoonekana ni lazima, kupokea rufaa na kukazia hukumu kutoka Baraza la Kata. Utaratibu wa usikilizaji wa mashauri . Kesi itaendeshwa kwenye eneo la wazi.. Mlalamikaji au mlalamikiwa anaweza kujieleza mwenyewe au kuwakilishwa na wakili au ndugu yeyote au mwanafamilia aliyeteuliwa na mhusika. Baraza litatumia lugha ya Kiswahili au Kiingereza kusikiliza mashauri kama mwenyekiti atakavyopendekeza, isipokuwa kumbukumbu na hukumu ya mashauri ya Baraza yataandikwa kwa lugha ya Kingereza.


 Baraza baada ya kusikiliza rufaa linao uwezo wa kuthibitisha, kutengua, kukataa au kurekebisha uamuzi uliotolewa na Baraza la Kata, kufuta shauri lililoamuliwa na Baraza la Kata, kuita na kuchunguza kumbukumbu za mashauri ya Baraza la Kata na kuagiza Baraza la Kata kupitia upya au kurekebisha uamuzi uliofanyika. Pia, baraza litahusika kutoa sababu za kufikia uamuzi huo.


Baraza la Ardhi na Nyumba la Wilaya hutekeleza hukumu zake lenyewe kwa kutumia madalali wake. Vilevile Baraza hili linasimamia utekelezaji wa hukumu za Baraza la Kata. Kwa sababu hiyo Baraza la Kata halina mamlaka ya kukaza hukumu zake lenyewe. vii. Ukataji Rufaa kutoka Baraza la Ardhi na Nyumba la Wilaya Upande wowote ambao haukubaliani na maamuzi au amri ya baraza unaweza kukata rufaa Mahakama Kuu ndani ya siku sitini (60) toka tarehe ya kusomwa hukumu, ikiwa kesi hiyo ilianzia Baraza la Kata na kwenda Baraza la Ardhi na Nyumba la Wilaya kama rufani.


Endapo shauri hilo lilianzia Baraza la Ardhi na Nyumba la Wilaya itabidi rufani ikatwe ndani ya siku 45 kwenda Mahakama Kuu. MAHAKAMA KUU Muundo wa Mahakama Kuu; kwa Mujibu wa Ibara ya 108 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, inatamka wazi wazi yakuwa kutakuwa na Mahakama Kuu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambayo kwa kifupi itaitwa “Mahakama Kuu”.


Ibara ya 109 inaelekeza kuwepo kwa majaji ambao ni wateuliwa wa Rais baada ya mashauriano na Tume ya Utumishi ya Mahakama. Majaji husikiliza na kutoa hukumu katika ngazi ya Mahakama Kuu na Mahakama ya Rufaa.


Usikilizaji wa mashauri Mahakama Kuu ina uwezo wa kusikiliza mashauri kwa mara ya kwanza kama ifuatavyo: 17 . Mashauri ya madai ya mali isiyohamishika yenye kiwango cha thamani inayozidi shilingi milioni hamsini (50,000,000) na mali inayohamishika inayozidi thamani ya shilingi milioni arobaini (40,000,000).


 Mashauri yote chini ya Sheria ya Uwekezaji ya mwaka 1997, Sheria za Ardhi za mwaka 1999 na Sheria ya Utwaaji wa Ardhi ya mwaka 1967 yanayohusisha serikali. Mashauri yote yanayohusiana na mashirika ya umma. Mashauri yoyote ya ardhi chini ya sheria yoyote iliyoandikwa ambapo mamlaka ya kusikiliza shauri hilo hayakupewa mahakama au baraza lingine. Uwezo wa Mahakama Kuu Mahakama Kuu ina uwezo wa kuamuru Baraza la Ardhi na Nyumba la Wilaya kutafuta ushahidi zaidi kukubaliana na maamuzi ya Baraza la Ardhi na Nyumba la Wilaya, kubadili na kubatilisha maamuzi ya awali, itakuwa mshauri mkuu wa Baraza la Ardhi na Nyumba la Wilaya na ina uwezo wa kukagua kumbukumbu zake wakati wowote na kutoa mwongozo kwa baraza hilo.


Ukataji rufaa kutoka Mahakama Kuu Upande wowote ambao hautaridhishwa na maamuzi ya Mahakama Kuu unaweza kukata rufaa katika Mahakama ya Rufaa ndani ya siku 30 kwa kuzingatia siku 14 za notisi ya kusudio la kukata rufaa. Kila rufaa itakayowasilishwa Mahakama Kuu itasikilizwa chini ya Jaji mmoja, pia rufaa inayohusu masuala ya sheria za kimila Mahakama Kuu ina uwezo wa kuelekeza swala lolote la sheria za kimila kwa mtaalamu au jopo lililoundwa na wataalamu wa mila. 


Mahakama hii inaundwa na Jaji Mkuu ambaye huteuliwa na Raisi kwa mujibu wa katiba ya Jamhuri ya Muungo wa Tanzania, Ibara 118 (2). Jaji Mkuu ndiye kiongozi wa Mahakama ya Rufaa na mhimili wa Mahakama za Tanzania kwa ujumla. Katika ngazi hii Rais akishauriana na Jaji Mkuu atateua majaji wa Mahakama ya Rufaa, ambao ni majaji waliotumikia kwa kipindi kisicho pungua miaka kumi na tano (15) katika Mahakama Kuu upande wa Bara na Mahakama Kuu ya Zanzibar.


Utatuzi wa Migogoro ya Ardhi Tanzania Rufaa: Mtu yeyote ambaye hataridhishwa na maamuzi ya Mahakama Kuu anaruhusiwa kupeleka madai kwenye Mahakama ya Rufaa. Kwa madai yoyote yanayotoka katika Baraza la Kata yatatakiwa kuambatanishwa na cheti kutoka Mahakama Kuu. Taratibu za uendeshwaji wa mashauri ya rufaa zitaongozwa na sheria na kanuni za Mahakama ya Rufaa.


Hapo huwa ndipo hitima ya migogoro ya ardhi safari ndefu, Je mkulima mdogo mdogo wa jembe la mkono anaweza kuvumilia safari yote hiyo? Kwa hakika kesi hiyo kama inapitia hatua zote hizo ni kazi kubwa na ndiyo maana taasisi nyingi za haki za wakulima zinashauri migogoro hiyo kutatuliwa katika hatua za mwanzo. Kusaidia jamii kujishughulisha zaidi na shughuli za uzalishaji mali na siyo kuketi katika vikao.Viongozi wa Wilaya na mikoa na kitaifa wanapaswa kuwa jirani sana na jamii  mathalani kuwachagua wajumbe wenye sifa kutoka ngazi ya kata ili kusaidia kutatulika kwa migogro hiyo mapema kama anavyofanya mkuu wa Mkoa wa Marogoro hivi sasa Martine Shingela.


makwadeladius@gmail.com

0717649257

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI