MWENYEKITI Chama cha waandishi wa habari za mazingira Tanzania(JET)Dr.Ellen Otaru amesema matumizi mabaya mazingira yanayofanywa na binaadam yanachangia wanyama na viumbe hai mbalimbali kupotea na hata baadhi yao kufariki.......Na Editha Karlo_ Dar es salaam
Hayo ameyasema kwenye mkutano uliofanyika hivi karibuni jijini Dar es Salaam uliowashirikisha waandishi 25 wa habari kutoka vyombo mbalimbali vya habari nchini.
Mkutano huo ulikuwa ukihusu uhifadhi,uwindaji haramu wanyamapori na usafirishaji kwa kupitia mradi wa USAID tuhifadhi Maliasili ambao unatekelezwa na chama cha waandishi wa habari za mazingira Tanzania(JET)kwa muda wa miaka mitano.
Alisema asilimia kubwa ya watanzania ni vijana na ndio mtegemeo la Taifa,mambo ya kijamii yanaongezeka kila siku lakini ardhi bado inaendelea kubaki hivyo hivyo hali inayopelekea kugusa maeneo ya uhifadhi maliasili,hivyo kuna haja ya kuangaliwa upya mipango miji na kuwepo kwa maeneo maalumu ya uhifadhi.
Aliwataka wanahabari baada ya mafunzo hayo kutumia kalamu zao kwa kuandika habari zitazoigusa jamii kuendeleza kuifadhi maliasili kwaajili ya vizazi vijavyo.
Kwa upande wake Mkurugenzi mtendaji wa chama cha waandishi wa mazingira Tanzania(JET)John Chikomo alisema kuwa waandishi wanayo nafasi kwa kutumia kalamu zao kwa kuandika habari habari za kuelimisha umma kuachana na matukio ya uwindaji haramu.
Chikomo alisema lengo la mafunzo hayo ni kuwajengea uwezo wanahabari wa kusimamia na kuandika habari za uhifadhi,uwindaji haramu na usafirishaji wa wanyama pori ili jamii iweze kufahamu changamoto kubwa inayoikumbuka sekta ya uhifadhi wa maliasili.
Mtaalamu kutoka mradi wa USAID Tuhifadhi maliasili Joseph Olila aliwataka waandishi wa habari kuwa mstari wa mbele kupaza sauti kwa jamii kwa kuandika habari zenye kuifanya jamii itambue mipaka yao na wanyamapori.
"Wanahabari nyinyi mnayo fursa ya kupaza sauti kwa umma katika hili suala la ushiriki wa kusimamia mchakato wa kupanga ardhi kwa manufaa ya wanyama,ili watu waelewe shughuli za kibinaadam hazipaswi kuzidi mipaka"alisema Olila
Naye Ofisa mtandao wa ufuatiliaji biashara ya wanyamapori Allen Mgaza wakati akiwasilisha mada yake alisema kuwa waandishi wanatakiwa kuibua biashara haramu za viumbe bahari na wanyama ambavyo vimepigwa marufuku lakini kuna baadhi ya wananchi wanaifanya kwa kujua au kwa kutokujua.
"Kuna viumbe bahari baadhi ni maarufu kuvifanyia biashara lakini vinauzwa mtaani,pia kuna watu wanauza mafuta ya simba kama dawa,kucha za simba,ngozi za chui na siyo rahisi kuwagundua,ila ninyi waandishi hiyo ni kama"tip"mnaweza ifuatilia na kuandika habari za kuelimisha jamii"alisema Mgaza
Nao waandishi wa habari za uhifadhi,uwindaji haramu wa wanyamapori na usafirishaji wameushukuru mradi wa USAID tuhifadhi Maliasili pamoja na chama cha waandishi wa habari za mazingira Tanzania(JET)kwa kuwapatia mafunzo hayo ambayo yameweza kuwajengea uelewa juu ya uhifadhi wa wanyama pori.
0 Comments