Header Ads Widget

WATU WAWILI MKOANI RUVUMA WANASAKWA NA JESHI LA POLISI KWA TUHUMA ZA KUWAUWA WAKE ZAO

JESHI la polisi mkoani Ruvuma linawasaka watu wawili  katika matukio tofauti kwa tuhuma za kuwashambulia kwa vipigo  wake zao na kuwasababishia vifo. mwandishi wa matukio daima Amon Mtega anaripoti kutokea Ruvuma

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jana kaimu kamanda wa polisi mkoani Ruvuma Pili Mande amelitaja tukio la kwanza limetokea Oktoba 31 mwaka huu majira ya mchana huko katika Mtaa wa Mateka manispaa ya Songea.

Mande alisema kuwa inadaiwa kuwa Marehemu huyo ambaye jina lake limehifadhiwa  kabla ya kifo chake alikuwa kwenye sherehe nyumba ya jirani yao akiwa amesimama na mwanaume mwingine kwenye sherehe hiyo na ndipo alipokutwa mme wake ambaye jina naye limehifadhiwa kwa sababu za kiuchunguzi zaidi.

Alisema kuwa  mume  alianza kumshambulia kwa kumshushia  kipigo katika maeneo mbalimbali ya mwili na kumsababishia Bandama kupasuka jambo ambalo lilipelekea kuvuja kwa damu nyingi hadi kupelekea kifo chake.

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma Mande alifafanuwa kuwa inadaiwa mtuhumiwa baada ya  kugunduwa kuwa ameuwa alimchukuwa mtoto wake na kwenda kumtelekeza kwa babaake mzazi ambaye jina lake limehifadhiwa  kisha baadae alikimbia na kutokomea kusikojulikana.

Aidha kaimu kamanda Mande alilitaja tukio la pili kuwa limetokea Oktoba 28 mwaka huu majira ya usiku huko katika kijiji cha Mageuzi Wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma ambapo mwanamke mmoja ambaye jina lake halikutajwa mwenye umri wa miaka 33 inadaiwa kuwa alipigwa na shoka kichwani kutokana na mume wake kumtuhumu mke wake kuwa anamahusiano ya kimapenzi na wanaume wengine.

Alieleza kuwa wapenzi hao walikuwa wametengana lakini siku ya tukio bwana alimraghai mpenzi wake wa kike kwa kumnywesha pombe kisha kwenda nae nyumbani kwake ambako baadae  alimpiga na shoka kichwani na kumsababishia kifo.

Mtuhumiwa baada ya tukio hilo inadaiwa kuwa aliuza mahindi na maharage ambayo alipata nauli kisha alikimbia na kutokomea kusiko julikana na polisi inaendelea kumsaka.

Jeshi la polisi kutokana na matukio hayo kukithiri mkoani humo limekemea na kulaani vikali kwa mtu yeyote atakayebainika kumshambulia kwa kumpiga mke wake au mume wake atachukuliwa hatua kali za kisheria bila kujali wadhifa wake kwa kuwa mashambulio hayo yanaleta madhara makubwa kwa familia na jamii kwa ujumla na si vinginevyo.

Katika hatua nyingine kaimu kamanda Mande alisema kuwa kwa wale wanaomiliki silaha kinyume na sheria amewataka wajisalimishe wenyewe kwenye vituo vya polisi vilivyokuwa jirani kuanzia Novemba mosi hadi Novemba 30 mwaka huu.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI