Uongozi wa Serikali ya Mtaa wa Bonyokwa umewataka wanawake wa mtaa na Kata ya Bonyokwa kuunda vikundi vya kijamii na kiuchumi vitakavyo wawezesha kupata mkopo wa asilimia 10 inayotolewa na Halmashauri zote nchini Tanzania kwa wanawake, vijana na walemavu Ili waweze kujiendeleza kimaisha......Na Fatma Ally MDTV Dar es Salaam
Wito huo umetolewa na Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Bonyokwa Shaaban Maliyatabu wakati alipokua akifungua kongamano la uwezeshaji wanawake kiuchumi liliandaliwa na uongozi wa serikali ya mtaa huo lengo ni kuwa na chombo chao ambacho kitakachoweza kuwa sauti yao.
"Lengo kubwa ni kuwawezesha wanawake waweze kukaa pamoja wawe na chombo chao kitakacho kuwa sauti yao kama ni wajasiriamali wakae pamoja, wabunifu ama watu wanaofanya ujasiriamali unaofanana ili tuweze kuwatambua na kuwashika mkono"amesema Maliyatabu.
Amesema kuwa, endapo watakua wakifanyakazi pamoja itakua rahisi kuweza kutambua changamoto zao na kufanyiwa kazi kuliko kuwa mmoja mmoja, kwani tuwaweza kuwatambua wangapi wana viwanda wanafanya nini wanakwama wapi Ili tuweze kuwashika mkono.
Hata hivyo, amesema mikopo ya Rais Samia ipo, ikiwa mtu mmoja hawezi kupata lakini wakiwa vikundi wanaweza kuwasimamia kama shida ni katiba, usajili kama utengenezaji wa miswada wanaweza kuwasimamia kupitia uongozi wa Serikali ya mitaa.
Amesema kuwa, dhamira ya kuwakutanisha pamoja wanawake hao kujiandaa na maandalizi ya mkutano mkubwa ambao utakwenda kufanyika mwezi ujao ambao umelenga kuwajengea uwezo na hatimae kuweza kuunda Umoja wa wanawake Bonyokwa (Bonyokwa Women Saccos)
"Ndio maana leo tumewaletea Taasisi mbalimbali na wawezeshaji ili waweze kuwapiga msasa katika eneo hilo, kwani tunaamini wanawake ni jeshi kubwa ukiweza kumsaidia ama kumuwezesha mwanamke, umelipa thamani na nguvu eneo hilo"amesema Maliyatabu.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Shirika la Ushindi Women Development Organization (UWODO) Phebby Mwaseba, amewataka wanawake wa Bonyokwa kuweza kujiunga na Shirika hilo Ili waweze kupata fursa mbalimbali zinazopatikana katika Shirika hilo.
Aidha amesema lengo la Shirika hilo ni kuwajengea uwezo wanawake kushiriki katika shughuli mbalimbali za maendeleo, kutoa elimu ya utetezi wa haki za wanawake pamoja na kuwawezesha wanawake kutambua kuheshimu na kufikia hatima za ndoto zao.
"Katika Shirika letu kuna fursa mbalimbali ambazo zinakua mtetezi wa wanawake katika changamoto mbalimbali anazozipitia ikiwemo kuelimisha jamii juu ya mapambano dhidi ya maambukizi ya VVU/UKIMWI , CORONA na magonjwa mengine"amesema Phebby.
Hata hivyo, amesema Shirika hilo huwafikia wanawake na akina mama kwa njia ya kuwatembelea au kuwakusanya pamoja Ili kuweza kuelimishana na kupeana mbinu mbalimbali juu ya ujasiriamali na kujikwamua kiuchumi Ili kuweza kupambana na changamoto za kimaisha katika jamii.
0 Comments