Na, Titus Mwombeki-MTDTV-BUKOBA.
Vijana mkoani kagera wameshauriwa kuingia darasani kusomea mpira wa miguu ili kuweza kupata maarifa zaidi kuhusu mpira huo na kuweza kukuza vipaji vyao.
Hayo yamesemwa na diwani wa kata ya Nshambya ambaye pia ni Mstahiki Meya wa Manispaa ya Bukoba Godson Gypson Rwegasira wakati akitoa neno baada ya kumalizika kwa fainali ya ‘King Rumanyika Cup’ iliyokutanisha timu mbili, timu ya Chuo cha King Rumanyika na timu ya Bunkango FC zote zikitoka kata ya Nshambya, Kabumbu iliyochezwa katika uwanja wa Kaitaba.
“Mpira sio kupiga tu vijana wanatakiwa waingie darasani ili wapate maarifa zaidi namna ya kucheza mpira kwa ustadi na sio kuingia uwanjani na kupiga tu kama vijana wengi wanavyowaza, mpira ni afya, elimu pia ni ajira kwahiyo unahitaji umakini na maarifa mengi”
Adha, Mstahiki Meya ameongeza kuwa michezo inaumuhimu sana kwa vijana kwani nje na kujenga afya pia inasaidia kuwaweka pamoja na kuweza kutambuana kama vijana.
“Lengo kubwa la kuanzisha mashindano haya nikuwaweka pamoja vijana ili waweze kufahamiana, kujuana na mwishowe niweze kuona nikwajinsi gani vijana hao wanaweza kupata mikopo ya vijana”.
Ameongeza kuwa kuhusu uhaba wa viwanja vya michezo katika Manispaa ya Bukoba suala hilo ameishaagiza maafisa mipango miji kwenda kubaini maeneo ya wazi ili kujenga viwanja vya michezo, na kusisitiza kuwa hadi kufikia mwezi Desemba viwanja vya michezo vitakuwa vimeisha karabatiwa.
Kwaupande wake Amon Robert mchezaji wa timu ya Bunkango FC amemshukuru diwani wa kata ya Nshambya kwa kuandaa mashindano hayo kwani wamejifunza mambo mengi ikiwemo kujuana pamoja na kuwajenga kinidhamu.
“Kupitia michezo inatusaidia sisi kama vijana kukutana mara kwa mara na kuwa wamoja kwani sisi sote ni vijana ambao tunaishi wote mtaani kwahiyo niwaombe vijana wenzangu yanaptokea mashindano mengine kama haya tuweze kujitokeza kwa wingi kushiriki mashindano hayo kwa pamoja”.
Kombe la King Rumanyika lilikuwa na jumla ya timu nane (8) zote zikiwa zimetoka katika kata ya Nshambaya ambapo timu ya Bunkango imefanikiwa kutwaa ubingwa baada ya kuifunga timu ya King Rumanyika FC mabao 3-1 mchezo ulioenda mpaka hatua za matuta, na mshindi kujinyakulia kitita cha shilingi 500,000 katika mashindano hayo yaliyoandaliwa na diwani wa kata ya Nshambya na mshindi wa pili amejinyakulia shilingi 300,000 huku mshindi wa tatu akijinyakulia shilingi 200,000.





0 Comments