Header Ads Widget

UKITEULIWA KUMBUKA KUNA KUTENGULIWA

Hayati Rais DKT John Magufuli 

“Jamani ninawashukuru sana kwa kuhudhuria kikao hicho nyinyi mliobaki nendeni mkafanya kazi, kwa kuwa leo ni Ramadhani wale ndugu zangu waislamu mmefunga na hati sie tusiofunga basi tutafuturu pamoja, karibuni(makofi yakisindikiza).” Nakumbuka hiyo ilikuwa ni sentensi yangu ya mwisho kuisikia katika jengo lile ambalo mara ya kwanza niliingia baada ya kuteuliwa na mara ya mwisho ni siku hiyo ya Mei 16, 2019 nilipotenguliwa.MWANDISHI WA MATUKIO DAIMA ADELADIUS MAKWEGA.ANACHAMBUA KUTOKA DODOMA


Niliamka katika kiti cha ukumbi huu huku kwa mkono kulia alikuwepo ndugu mmoja ambaye alifahamika kama Maheji ambaye wakati huo alikuwa Mkurugenzi wa Jiji la Tanga nikaomba njia kupita katika ukumbi na kutoka nje, ukumbi siku hiyo huo uliojazwa na viongozi wakuu karibu wote, kwa CCM siku hiyo ikiwakilishwa na Ndugu Polepole, baadhi ya Mawaziri, Wakuu wa Mikoa, Makatibu Tawala, Wakuu wa Wilaya, Makatibu Tawala wa Wilaya, Wakurungenzi wa Halmashauri zote nchini, Jaji mmoja na baadhi ya viongozi wa taasisi kadhaa ambao walitoa mada katika kikao hicho.


Nilitoka zangu hadi getini lililo jirani na  bahari na kukutana na wahusika wa eneo hilo waliovalia suti nadhifu.

“Mkurugenzi wa Mbozi naomba namba yako yako ya simu” nilimjibu kuwa kaka uteuzi wangu umetenguliwa kikaoni. Kijana huyu wakati naingia asubuhi getini alinidokeza kuwa anazaliwa Wilaya ya Mbozi huku akinitajia kata na kijiji ambapo wazazi wake wanaishi na inaonekana alikuwa akinifahamu vizuri. Wakati natoka nilivyomueleza tu kilichotokea alikaa kimya hakusema neno wala ishara yoyote kwangu bali aliniuliza aina ya simu yangu na kunipatia maana simu zote zilihifadhiwa kwake wakati wakuingia ukumbini.


Gari la Wilaya ya Mbozi nililokuja nalo lilikuwa kandokando ya Barabara ya Baraka Oboma (zamani Ocean Road) nilimueleza dereva kilichotokea na yeye alichanganyikiwa mno ilibidi nimtafute dereva mwingine wa serikali kutoka taasisi fulani ambayo niliwahi kufanya kazi ili aokoe jahazi hilo ili kuanza safari ya Songwe.


Kilichokuwa kinanipeleka huko ni kwenda kukabidhi kama nilivyokabidhiwa baada ya kuhamia huko, ninapaswa kukabidhi kwa wahusika. Dereva huyu alipatikana na tukaanza safari ya kwenda Mbozi. Nikiwa njiani sasa tayari wahusika wa Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu wa wakati huo walishatangaza rasmi kuwa mimi na Mkurugenzi wa Uyui Bi Hadija Makuhani tayari uteuzi wetu umetenguliwa na nafasi hizo zitajazwa baadaye


Kurugenzi hii ilikuwa ikifanya kazi kwa haraka mno na kwa wakati, lakini binafsi siamini  kama haraka hiyo ya kutangaza tenguzi au teuzi kama inalingana na uwezo wao wa kuhimili kutenguliwa kama wao pia wangelitenguliwa, lakini ninalolitambua ni moja tu lakini wao piawapo kibaruani wakitimiza wajibu angalau watoto wao mkono uende kinywani.


Huku nikiyafuatilia maoni ya wasomaji wa habari hiyo waliyokuwa wakitoa katika mitandao ya kijamii kila mmoja akisema yake.


Wengine wakitumia kutumbuliwa huku wakishutumu hata maumbile yetu baina ya mimi na Bi Hadija Makuhani ambaye alikuwa Mkurugenzi wa Uyui namna tulivyo mbona huyu mnene sana na wengine mbona huyu kapauka na kakonda sana. Lakini hayo yalikuwa maoni yao.


Binafsi sikuwa karibuna Bi Makuhani na kwa sasa sifahamu alipo lakini bado namtafuta hadi leo maana ni miaka miwili sasa waswahili wanasema kuwa wale wanaokwenda pamoja mkoleni/jandoni ni vizuri kukumbukana hata kusimuliana habari za maisha ya mkoleni/jandoni yalivyokuwa.


Kwa kuwa safari ilikuwa ndefu si kama safari ya siku zote maana sasa nilikuwa na dereva mgeni lakini dereva wa Halmashauri ya Mbozi kidogo aliweza kuwa na nguvu za kuweza kuongea lakini nilikuwa na hofu moja isije akalitumbukiza gari hii Land Cruezer V8 Old Model katika mitalu alafu ikaleta matatizo na gari lenyewe lilikuwa na mizengwe mingi tangu nilipoanza kulitengeneza kwani awali lilikuwa juu ya mawe.


Safari iliendelea hadi tukafika Mafinga, hapo tulipumzika maana palikuwa na mkahawa ulikuwa barabarani ulikuwa unamilikiwa na kaka mmoja wa mwenyeji wa Muheza Tanga. Alikaribisha akasema mjomba pole sana kwa changamoto na ndiyo maisha yalivyo. Mandhari ya pale ilininyima raha kwa kuwa sasa kila mmoja alishafahamu kuwa nimetumbuliwa lakini nilijipiga moyo konde, tulikaa pale kwa dakika kadhaa alafu tukaendelea safari ya Mbozi.


Ilipofika saa mbili ya asubuhi sasa tulikuwa tupo Mbalizi,  sasa dereva wa Halmashauri  Mbozi nilimuomba aendeshe gari huku tukiliacha eneo la Mbalizi ambalo wakati huo lilionekana kuwa eneo lenye biashara nyingi na kuchangamka. Ndani ya gari mwezetu mmoja ambaye alikuwa mwanamke akiuliza kwanini makao makuu ya Mbeya Vijiji yasingekuwa Mbalizi?Tukilijadili hilo mara alipiga simu na Afisa Usafirishaji wa Wilaya ya Mbozi akiuliza juu ya Gari ya Serikali lipo wapi kwa sasa? Alijibiwa na dereva kuwa sasa tupo Mpakani wa Mbeya na Songwe. Akasema.


“Tumejulishwa na Katibu Tawala wa mkoa ameagiza gari hiyo ipelekwe katika yadi ya mkoa.”


Basi tulipofika Mbozi dereva wa halmashauri alienda kukabidhi na sikuonana naye tena, sikujua kilichoendelea maana ya huku yalikuwa si yangu tena. Nilielekea Halmashauri na tayari vitabu vya kukabidhiana vilikuwa tayari na mie kufanya hivyo japokuwa hakukuwa na hali nzuri huku kukiwa na maagizo mengi juu ya makabidhiano hayo.


Mkuu wa idara mmoja aliniambia kuwa watumishi wapo ukumbini wanataka kuniaga lakini baadaye niliambiwa kuwa kikao hicho kimeagizwa kisifanyike, huku watumishi wakikimba huku na huku.


Basi nilitoka ofisi ya halmashauri na kurejea vilipo vyombo vyangu na baadhi  madereva wa Halmashauri ya Mbozi walikuja kunisaidia kufunga vyombo hivyo wakishirikiana na kijana mmoja ambaye alikuwa amehitimu kidato cha nne lakini hakufanya vizuri katika mtihani huo ambaye nilimfahmu kutokana na mimi kuwa mfugaji wa mbuzi. Mbuzi zangu kadhaa na nilikuwa na mabeberu makubwa mawili ambayo kwa mbegu yalikuwa hodari sana.


Mabeberu haya yalikuwa yakikimbilia kwa akina Milton Obote kufuata majike na mara zote kijana huyu hakuwahi kuzificha mbuzi zangu. Kwa kuwa tangu alipokuwa shuleni sekondari Vwawa alikuwa akipita jioni alikuwa akiniona nikizichunga mbuzi zangu mara baada ya saa za kazi. Alitambua kuwa mbuzi zile za mkurugenzi. Lakini pia ifahamike kuwa wafugaji huwa wanatambuana kama walivyo walevi.


Kazi ya kufunga vyombo iliendelea lakini nitavisafirishaje hadi kwetu Pwani? Na tarehe yenyewe 17, basi niliwasiliana ndugu yangu mmoja aliye ughaibuni na kunijulisha niwasiliane na mtawa mmoja wa Kanisa Katoliki ambaye aliniwezesha.


Nikiwa nafunga mizigo yangu watu kadhaa waliweza kuja kuniaga wakati wa usiku hasa watumishi wa kada ya chini, watumishi wa kada ya juu hawakujaliwa kufika.  Machoni  pa wengi viongozi wanaotenguliwa ni wakosaji na watovu wa nidhamu adhabu hiyo ya kutenguliwa inaonekana ni haki yake mhusika.


Watumishi wa kada ya juu wanatambua kuwa aliyetenguliwa sasa siyo kiongozi wao tena wansubiri kiongozi mpya ili wawe salama binafsi nasema ni sahihi  kabisa wao kumkwepa aliyetenguliwa.Watumishi wa kada ya chini kama ulikuwa nao jirani vijidokezo vyao unavipitisha havikwamikwami watakupenda sana, watakulilia sana lakini kilio chao hakitaweza kusikilizwa na binadamu labda ni mola peke yake.


Wakati huo Wilaya ya Mbozi ilikuwa na shekhe mkuu wa Baraza la Waisalamu Tanzania (BAKWATA) ambaye alifahamika kama Shekhe Mbwana kweli aliwasiliana nami baada ya tukio hilo na aliendelea kuwasiliana nami kwa muda mrefu, akinielekeza baadhi ya mambo ya kutiana moyo. Kumbuka kuwa mimi sikuwa muumini wake lakini kiongozi huyu wa BAKWATA alikuwa mtu muungwana sana.


Jambo la tatu lilonishangaza zaidi lilikuwa ni mheshimiwa mmoja aliyefahamika kama Bahati Mbugi ambaye wakati huo alikuwa diwani wa CHADEMA kata ya Ichenjezya na kwa Halmashauri alikuwa mjumbe wa Kamati ya Elimu Afya na Maji. Mheshimiwa huyu hakuwa na urafiki na mimi lakini ninachoweza kukumbuka alikuwa akija kuomba madawati na vifaa vya ujenzi na alikuwa akipatiwa. Alikuwa akionesha kuwapenda sana wapiga kura wake.


Kata yake ilikuwa ni miongoni mwa kata ya mjini na ndiyo ilikuwa makao makuu ya wilaya na mkoa wa wakati huo. Alifika kunisaidia kufunga vyombo vyangu vizuri na kwa kuwa likuwa mwenyeji alinitafutia Lori la kubeba vyombo vyangu na nililipia na safari ilianza na kurudi kwetu.


Ujio wa diwani huyu ulinipa picha ambayo sikuilewa huyu hakuwa diwani wa chama  tawala ilikuwaje alikuwa ni mtu wa hisani namna hiyo? Wako wapi madiwani wengine? Au ndiye ile simulizi ya wakuu wa idara?. Hakikisha ukiwa kiongozi pahala popote wewe tenda wema kwa wote bila kubagua. Siyo kutenda wema kwa kungoja hisani bali wema ni jambo la msingi sana kwa kila mmoja wetu.


Pengine wale marafiki zangu wote wa CCM labda niseme walimtuma mheshimiwa huyu diwani wa CHADEMA aje kuwawakilisha labda! Hapa najaribu kuwaza tu.


Kingine kikubwa nilichojifunza Mbozi ni wilaya ya jamii ya Watanzania wapenda maendeleo sana, wachapa  kazi, ukiwashirikisha jambo  hawezi kuwa vigeugeu. Ukisema kuwa wao wajenge boma la zahanati na mkurugenzi uwapelekee mabati lazima watatekeleza ilimradi serikali iwe na kauli thabiti. Tatizo la wilaya hii ni baadhi tu ya watu waliojiingiza katika siasa. 


Kweli nilisafiri na kufika nyumbani kwetu salama salimini, ninaweka kalamu yangu chini kwa kusema kuwa unapoteuliwa kumbuka kuna kutenguliwa pia.


makwadeladius@gmail.com

0717649257.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI