Akizungumza na Watanzania kupitia vyombo vya habari, Waziri wa Madini, Dotto Biteko alisema kabla ya uhuru shughuli za madini na biashara ya madini hazikuwa kubwa.
“Ikilinganishwa na tulipotoka, hivi sasa Taifa letu lina migodi mikubwa tisa, pia ipo migodi takribani 28 ya uchimbaji wa kati na mingine mingi ya uchimbaji mdogo wa dhahabu, almasi, madini ujenzi, madini ya viwandani na ya vito vya thamani,” alieleza Biteko.
Akiielezea migodi mikubwa, Waziri huyo alihabarisha kwamba migodi sita ni ya dhahabu, mmoja wa almasi, mmoja wa tanzanite na mmoja wa makaa ya mawe.
“Hadi kufikia Septemba 2021, Leseni hai ambazo zimeshatolewa za utafutaji wa madini ni 1,044, leseni 15 za uchimbaji mkubwa, leseni 161 za uchimbaji wa kati, leseni 34,000 za uchimbaji mdogo na leseni 1,561 za biashara ya madini,” alidokeza Waziri Biteko.
Pamoja na hayo, alibainisha kuwa Tanzania ina jumla ya masoko ya Madini 42 na Vituo vya Ununuzi wa Madini 59 katika mikoa mbalimbali na kwamba mchango wa sekta hii kwenye Pato la Taifa ni asilimia 6.7 kwa mwaka 2020 kutoka asilimia 3.4 mwaka 2015.
“Wakati katika mwaka 2020 Sekta ya Madini ilichangia asilimia 6.7 kwenye Pato la Taifa, hivi karibuni mchango wa sekta umeongezeka hadi kufikia asilimia 7.7 katika robo ya pili mwaka 2021 (Aprili-Juni),” alifahamisha Biteko.
Sambamba na hayo, Waziri Biteko alieleza jitihada zilizofanywa na Serikali kufikia mafanikio hayo ikiwa ni pamoja na kutunga sheria mbalimbali zinazosimamia madini, kuanzisha taasisi zinazosimamia sekta hiyo pamoja na kuanzisha kozi zinazohusiana na madini kwenye vyuo mbalimbali nchini.
“Kuanzia miaka ya 1965 mpaka 1975 Bunge lilipitisha Sheria ya ‘The National Investment Promotion and Protection Act’ ambayo ilisimamiwa na Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC) kwa kuendeleza shughuli chache za uchimbaji na biashara ya madini,” alisema kiongozi huyo.
Aidha, alifahamisha kuwa mwaka 2009 Serikali ilitunga upya Sera ya Taifa ya Madini na kufuatiwa na Sheria ya Madini ya Mwaka 2010 na kwamba mnamo 2017 yalifanyika marekebisho makubwa katika Sheria ya Madini ya Mwaka 2010 kupitia Sheria ya Marekebisho ya Sheria mbalimbali Na.7 ya mwaka 2017.
“Mabadiliko hayo pia yalilenga kutambua haki ya ushiriki wa Serikali (Government participation) katika shughuli zote za uchimbaji, uchakataji na uchenjuaji wa madini na umiliki wa hisa kwa asilimia 16 (16% non dilutable free carried interest) katika makampuni ya uchimbaji na Serikali kuwa na Uwezo wa kuongeza ushiriki (Umiliki) mpaka kufikia asilimia 50 kupitia thamani ya vivutio vya uwekezaji na kikodi alivyopewa mwekezaji,” alieleza Biteko.
Baadhi ya taasisi zilizoanzishwa ili kusimamia sekta ya madini ni Wizara ya Madini, Shirika la Madini la Taifa (STAMICO), Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST), Kituo cha Jemolojia Tanzania (TGC) na Chuo cha Madini (MRI) ambacho ni miongoni mwa vyuo vinavyotimiza maono ya Baba wa Taifa Hayati Julius Kambarage Nyerere aliyetaka Watanzania wawe na elimu ya kusimamia rasilimali ya madini
0 Comments